Waziri mkuu aagiza mhandisi achukuliwe hatua ....soma habari kamili na matukio360....#share

Na Mwandishi Wetu, Mara

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemkabidhi Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, Mhandisi Obetto Sasi kwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Josephat Kandege baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Ofisi ya waziri mkuu, ametoa uamuzi huo jana jioni wakati aliposimamishwa na umati wa wananchi kwenye mji Mdogo wa Shitari alipokuwa njiani kuelekea kwenye kijiji cha Bubombi wilayani Rorya.

“Hatuwezi kuwa na mtumishi wa aina hii ambaye kila eneo tunakutana na changamoto za maji huku kukiwa hakuna hatua zinazochukuliwa licha ya Serikali kutoa fedha, hivyo namuagiza Katibu Tawala wa Mkoa alete mhandisi mwingine wa maji.”

Pia Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo kwenda wilayani Rorya na kukagua mradi wa maji katika mji Mdogo wa Shirati na kuona namna ya kuutekeleza.

Amesema kwa sasa Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo. Kampeni hiyo  inalenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo itawachukulia hatua wote watakaokwamisha miradi ya maji.



Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alimueleza Waziri Mkuu kwamba changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika mkoa huo inatokana na watendaji wa idara hiyo kutokuwa na uwezo wa kutosha kiutendaji.


Wilaya ya Rorya inatekeleza miradi 11 ya maji ya bomba kupitia Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RWSSP) katika vijiji vya Kinesi, Randa, Utegi, Mika,Kirogo, Nyihara, Kisumwa,Nyamkonge, Nyambori, Gabimori na Marasibora.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search