nEWS: Wizara ya Fedha na Mipango yaja na kanuni za usafirishaji, uingizaj na utoaji nje fedha taslimu...#share
WIZARA ya Fedha na Mipango imeandaa Kanuni za taarifa
za Usafirishaji na uingizaji wa fedha taslimu kutoka na kwenda nje ya nchi ambapo wasafirishaji wa fedha taslimu na
wasafiri wote wanaotoka au kuingia nchini, watatakiwa kutoa taarifa za fedha
taslimu wanazosafirisha ikiwa fedha hizo zinalingana au zinazidi kiasi cha dola
za kimarekani elfu kumi (USD 10,000).
Akizungumza leo wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku
mbili ya maandalizi ya utekelezaji wa Kanuni hizo, Kamishna na Mtendaji Mkuu wa
Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) Onesmo Makombe amesema utekelezaji wa
kanuni hizi, pamoja na mambo mengine utaiwezesha nchi kuwa na takwimu za
usafirishaji fedha taslimu.
“Takwimu hizo zitakazosaidia pamoja na mambo mengine
kubaini vitendo vya kihalifu, kupunguza utoroshaji wa mitaji na kuhakikisha
kuwa tunapunguza kama siyo kumaliza kabisa usafirishaji wa fedha zitokanazo na
uhalifu au/na fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi” amesema Makombe.
Aidha kanuni hizo zimeweka
adhabu zitakazochukuliwa dhidi ya wale watakabainika kutaka kupita na fedha
zinazolingana au zinazozidi kiwango kilichowekwa bila kutoa taarifa au
watakaotoa taarifa za uongo.
Amezitaja adhabu hizo kuwa
ni pamoja na kukamatwa kwa fedha taslimu walizonazo na kuchukuliwa hatua
nyingine za kisheria kama vile kufunguliwa mashtaka.
“Wahalifu pamoja na mambo mengine, wanapenda kusafiri
na fedha taslimu kwani wanaogopa kutumia benki kutuma fedha kutokana na umakini
unaoongezeka katika benki na udhaifu unaoweza kuwepo mipakani” Alisisitiza Bw.
Makombe.
Kamishna huyo amewaasa washiriki wa warsha hiyo
kutekeleza jukumu hilo kwa uadilifu na uaminifu mkubwa ili kuziba
mianya yote ambayo wahalifu wanaweza kuitumia kutimiza kusudi lao ovu na
kuhatarisha usalama wa nchi.
Kutokana na umuhimu wa ushiriki wa wadau mbalimbali
katika utekelezaji wa kanuni hizo warsha hiyo imejumuisha washiriki kutoka
taasisi mbalimbali wengi wao wakiwa ni maafisa forodha.
Washiriki hao wametoka Wizara ya Fedha na Mipango,
Wizara ya Fedha na Mipango-Zanzibar, Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Afrika Mashariki na kikanda, Mamlaka ya Mapato Tanzania na vikosi vya ulinzi na
usalama
Wengine ni Bodi ya Mapato Zanzibar, Kikosi Maalum cha
Kuzuia Magendo-Zanzibar, Shirika la Posta, Benki kuu ya Tanzania, Ofisi
ya Mkurugenzi wa Mashitaka-Zanzibar, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka-Tanzania
Bara Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania Bara na Zanzibar, Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania, Idara ya uhamiaji na Kitengo cha Kudhibiti Fedha
Haramu.
Mwandishi Wetu
No comments:
Post a Comment