PROFESA MBARAWA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA USIKU KAMBI YA SOGA YA UJENZI WA RELI YA KATI

WAZIRI wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amefanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa Kituo cha Soga, Wilayani Kibaha , mkoani Pwani ili kujiridhisha na utekelezaji wa masharti ya mkataba kati ya Serikali na Kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki kwa ajili ya kufanya kazi saa 24 ili kukamilisha ujenzi wa reli hiyo kwa wakati.

Katika ziara hiyo Profesa Mbarawa, licha ya kuwakuta baadhi ya Makandarasi na wasimamizi wakiwa kazini pia akabaini kuwepo kwa wasimamizi wachache wasiotosheleza na hivyo kuagiza kuongezwa kwa wasimamizi kutoka watatu waliokuwepo hadi kufikia 15.

"Natoa agizo kwa uongozi wa Shirika la Reli nchini (TRC), kuongeza wasimamizi wa mradi huo haraka iwezekanavyo ili kazi ya usimamizi iweze kufanyika kwa umakini na kwa muda wa saa 24", amesisitiza Prof.Mbarawa .

Aidha Waziri Prof. Mbarawa, amesema ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge)’SGR’ kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro yenye urefu wa KM 300 ambapo kati ya hizo KM 205 ni eneo la njia ya reli na nyingine 95 ni za kupishana na mradi huo utagharimu kiasi cha Shilingi Trilioni 2.79.

Profesa Mbarawa ameongeza reli hiyo ya kisasa inayotumia umeme itakuwa na uwezo wa kusafiri kwa mwendokasi wa KM 160 kwa saa kwa treni ya abiria na , treni ya mizigo itakuwa na uwezo wa kusafiri kwa KM 120 kwa saa na kubeba mizigo tani 10,000 kwa wakati mmoja.

Pamoja na hayo amesema kuwa kipande cha reli kingine kitakachojengwa ni kutoka Morogoro-Makutupola chenye urefu wa KM 422, na hivyo kufanya jumla ya KM 722 kutoka mkoani Dar es Salaam hadi Makutupora na mradi huo utagharimu kiasi cha zaidi ya Shilingi Trilioni 7 na fedha zote zitagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.

Hata hivyo ametumia fursa hiyo kumtaka mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo kupitia Meneja mradi, Kemal Artuz kuogeza kasi ya ujenzi ili kufikiwa makubaliano ya kukamilishwa kwa wakati ili kuwezesha watanzania kunufaika na matunda hayo.

Kwa upande wake Mhandisi Msimamizi wa Mradi huo, Josephat Rutaihwa amesema, kazi za ujenzi huo zinaenda kwa kasi kutokana na vifaa kuwepo eneo la mradi.

Mhandisi huyo amemhakikishia Waziri kuwa kazi hiyo inakwenda kama ilivypoangwa na kwamba mradi huo utakamilishwa ndani ya mkataba Novemba 2, 2019.


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search