Brighter Monday, Zoom Tanzania yajadili jinsi kuwezesha waajiriwa kupata fursa za kazi…soma habari kamili na matukio360…#share


Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam

MITANDAO ya Brighter Monday na Zoom Tanzania imekutana kujadili jinsi ya kuwezesha waajiriwa kupata fursa za kazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Brighter Monday na Zoom Tanzania Mili Rughani akizungumza wakati wa mkutano leo jijini Dar es Salaam.

Pia kuangalia namna waajiri wanavyoweza kupata fursa ya kutangaza nafasi za kazi na kuwafikia watu wengi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano huo Mkuu wa Masoko wa mitandao hiyo Elisha Simon amesema, lengo lao ni kuona jinsi ya kutatua changamoto kwa waajiri na waajiriwa. 

“Kilicho tukutanisha hapa ni kwamba mitandao hii imekutana ili kuangalia namna ya kuwezesha waajiriwa kupata fursa zaidi za kazi na kwa urahisi, lakini pia waajiri wapate nafasi ya kutangaza kazi zao na kufikia watu wengi,” amesema Simon.

“Kwa mfano sasa hivi kinachotokea ni kwamba, mwajiri akitangaza kazi yake kupitia Brighter Monday itatokea na Zoom pia kwa bei hiyo hiyo,” ameongeza.

Simon amesema kuwa kwa sasa fursa za ajira zinazotangazwa Brighter Monday zitaonekana moja kwa moja pia kwenye mtandao wa Zoom Tanzania.

Ameongeza kwamba kwa mtua atakayeomba kazi atakuwa akiona mchakato mzima ikiwa ni pamoja na kuona hatua ambayo CV yake imefikia. Lakini pia utasaidiwa namna ya kuiweka CV katika muundo mzuri.

Kwa upande wake Mhadhiri  Mwandamizi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (Udsm) na Mwenyekiti wa Wanataaluma wa chuo hicho ( UDASA) George Kahangwa amesema kuwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu wanapata changamoto nyingi kuhusiana na masuala ya ajira.

Amesema  miongoni mwa changamoto hizo ni kukosa sifa zinazotakiwa na waajiri.

“Kwa mfano hivi karibuni waajiri walisema asilimia 50 ya vijana wanomaliza vyuo vikuu Afrika Mashariki hawana sifa za kuajiriwa, hawaajiriki, kwa hiyo hii ni changamoto kwa vijana wenyewe na nichangamoto pia kwa taasisi ziwatayarishe kabla hawajaingia kwenye ajira,” amesema Kahangwa.

Aidha amezitaka taasisi na makampuni yanayoajiri kutoa ushirikiano katika kuwajenga vijana kwani hawawezi kupata mtu mwenye sifa wanazozitaka kama na wao hawatakuwa wadau kushiriki katika kutatua changamoto hiyo.

Naye Joyce Nangai kutoka Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) ameunga mkono kazi inayofanywa  na Zoom Tanzania na Brighter Monday kwani watarahisisha maisha kwa waajiri na wanaotafuta kazi.

“Kwa hiyo sisi kama chama cha waajiri tunaamini kabisa kwamba itawasaidia waajiri wengine na pia watu wanaotafuta kazi kuweza kupata kazi kirahisi na pia itasaidia kupunguza gharama ambazo waajiri wanazipata katika kuhakikisha kwamba wanapata wafanyakazi,” amesema.




About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search