Samia ateta na Balozi wa Ufaransa nchini...soma habari kamili na matukio360...#share
Na
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAKAMU
wa Rais Samia Suluhu Hassan leo
amekutana na kuzungumza na Balozi mpya wa Ufaransa nchini Frederic Clavier
ambaye aliongozana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa
(AFD) Emmanuel Baudran.
Makamu wa Rais Samia Suluhu
Hassan akizungumza na Balozi wa Ufaransa nchini Frédéric CLAVIER ofisini kwa
Makamu wa Rais Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo ambayo
yamefanyika Ofisini kwa Makamu wa Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam, Balozi Clavier amewasilisha
salaam za Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa Rais John Pombe Magufuli na kusema “Rais wa Ufaransa ana uhakika na
Tanzania ijayo na anaunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na Rais
Magufuli”
Balozi huyo mpya wa Ufaransa
nchini ambaye amekutana na kuzungumza na Mheshimiwa Makamu wa Rais aliipongeza
Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika masuala mbali mbali ya Kimataifa na
kusema “Tanzania ni nchi yenye utulivu na Amani kitu ambacho kinaipa taswira
nzuri Umoja wa Mataifa”.
Balozi amemjulisha Makamu wa Rais
kwamba Ufaransa imekusudia kuimarisha uhusiano zaidi na Tanzania wa Uchumi na
Siasa na kuanzisha majadiliano mbali mbali katika masuala ya
Mazingira,Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Balozi Clavier amemjulisha Makamu
wa Rais kuwa mwezi ujao kutakuwa na ugeni wa wafanya biashara kati ya 30 au 40
kutoka nchi ya Ufaransa ambao watakuja kujionea fursa mbali mbali za kibiashara
na uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania.
Amemuelezea Makamu wa Rais azma
ya Ufaransa kushirikiana na Vyuo Vikuu vya Tanzania katika kuanzisha na
kuendesha kozi mbali mbali kwa manufaa ya pande zote mbili.
Mwisho aliipongeza Serikali kwa
mapambano dhidi ya rushwa na urasimu jambo litakalo wavutia wawekezaji wengi
nchini.
Aidha, Emmanuel Baudran
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa alisema Shirika lao
linakusudia kuanzisha kiwanda cha vifaa vya umeme wa jua (solar) mkoani
Shinyanga pia shirika hilo limeshafanya miradi ya uboreshaji maji taka katika
manispaa ya Temeke na wanaendelea na mikakati ya uanzishwaji wa miradi mingine.
Kwa upande wake Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alimshukuru na kumpongeza
Balozi wa Ufaransa kwa kazi nzuri wanazofanya hapa nchini.
Alimhakikishia kwamba Serikali ya
Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano kwa mambo yote muhimu yenye maslahi kwa
wananchi.
Wakati huohuo Makamu wa Rais
alikutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini Mhe. Michael
Danford.
No comments:
Post a Comment