Video: IGP Sirro aanza saka-saka ya wauaji Kibiti; Mgambo akiuawa kinyama nyumbani kwake !!

Kamishna Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Tanzania, IGP Simon Sirro, jana alifanya ziara Wilayani Kibiti, Mkoani Pwani kuwafariji na kutathmini hali inayoendelea ya mauaji ya Askari na raia wasio na hatia.


Katika ziara yake hiyo ambayo aliongozana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Masauni, Sirro alikemea vikali mauaji hayo na kuwataka wanouhisika kuacha mara moja akionya mkono wa Sheria hautaacha hali hiyo iendelee. 

Ziara ya Sirro pamoja na mambo mengine muhimu, Ilikuwa ni kuitikia wito wa wazee wa maeneo hayo ambapo aliwatoa hofu wanakibiti na maeneo ya jirani kuishi kwa amani na kuwaomba ushirikiano wa taarifa muhimu zitakazosaidia kuwatia mkononi wahalifu...


Wakati huo huo kabla ya ziara hiyo ya IGP, maeneo ya Kibiti na Ikwiriri,... Kumeripotiwa mauaji mapya yaliyotokea usiku wa kuamkia jana ambapo mkazi mmoja wa eneo la Kifuru katika Kitongoji cha Kazamoyo kilichopo Ikwiriri wilayani Rufiji Mkoani Pwani   aitwaye Erick Mwarabu (37) ameuawa kwa kupigwa risasi usiku akiwa kwake.

Watu wa karibu katika eneo hilo wamesema marehemu huyo aliyekuwa ni Askari Mgambo alipigwa risasi tatu alipokuwa amejificha chini ya kitanda chake.

Mkazi mmoja wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Simon alisema watu hao wanaosadikiwa kuwa ni majambazi walivunja mlango wa nyumba yake saa 9 usiku kisha kuingia ndani na kutekeleza mauaji hayo.

Simon alisema watu baada ya kuingia ndani walipitiliza moja kwa moja hadi kwenye chumba chake ambapo walimkuta mkewe marehemu na kumhoji alipo mumewe.

Alisema baada ya kuona mkewe hataji mahali alipo mumewe walianza kumtafuta ndani ya nyumba yake na kufanikiwa kumuona marehemu akiwa amejificha chini ya kitanda chake.

Alifafanua kuwa watu hao baada ya kumuona akiwa amejificha uvunguni mwa kitanda walimpiga risasi kisha kutokomea zao.

Alisema watu hao mara baada ya kutekeleza maji hayo hawakuchukua kitu chochote lile.

Mganga mkuu wa kituo cha Afya Ikwiriri Dr Iddy Malinda alisema katika uchunguzi walioufanya walibaini marehemu alikuwa na majeraha matatu katika maeneo tofauti ya mwili wake.

" katika uchunguzi tuliofanya tumebaini marehemu alikuwa na majeraha matatu,mawili yalikuwa mbavuni upande wa kulia na moja kichwani" alisema.

Alieleza kuwa katika jeraha la kichwani marehemu alipigwa risasi upande wa kushoto wa shingo yake iliyoharibu kichwa chake.

Alifafanua kuwa mwili huo tayari umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi.

Awali akiongea tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani Onesmo Lyanga alisema Polisi walikuwa wakiendelea kufuatilia - mcl online na Ayo Tv

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search