UTAFITI TWAWEZA: Asilimia 74, wananchi wasema vigogo nchini wako juu ya sheria.....#share


UTAFITI wa  ‘Hapa usalama tu’  uliotolewa na taasisi ya Twaweza leo jijini Dar es Salaam unaonesha kuwa idadi kubwa ya vigogo wanaofanya makosa mbalimbali hawafikishwi katika vyombo vya sheria, badala yake wananchi wa kawaida wanaofanya makosa ndio hukamatwa na kuchukuliwa hatua.


Katika picha ni Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza Aidan Eyakuze.

Unaonesha kuwa asilimia 74 ya watu 1,805 waliohojiwa maeneo mbalimbali nchini katika kipindi cha Machi 31 hadi Aprili 17 mwaka huu, walikiri kuwepo kwa jambo hilo na kuonesha mashaka juu ya haki kutendeka katika makundi mbalimbali ya watu wenye nguvu katika jamii.

Utafiti huo pia umebainisha kuwa wananchi hawaombi msaada wa polisi, hasa pale wanapokuwa wahanga wa uhalifu.

“Ni mwanananchi mmoja tu kati ya wanne sawa na asilimia 26 anayeomba msaada polisi. Hata hivyo idadi hiyo inatofautiana kutokana na makundi mbalimbali,” alisema Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza wakati akiwasilisha matokeo ya utafiti huo ambapo wananchi walihojiwa kwa njia ya simu.

Amebainisha kuwa makundi yalioonesha kuwa na uwezo wa kuomba msaada wa polisi ni;  matajiri asilimia 42, wakazi wa mjini asilimia 41.

Amesema wananchi wengine ambao ni asilimia 66 kabla ya kwenda polisi, huanzia  kwa mwenyekiti wa kijiji au mtaa.
Amesema asilimia 21 ya waliohojiwa walisema hawatatoa taarifa za uhalifu zilizolenga kaya zao na asilimia 8 walisema uhalifu kwenye jamii zao hautaripotiwa.

 “Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,805, kutoka maeneo mbalimbali Tanzania Bara. Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya, “alisema Eyakuze.

Aidha ameeleza kuwa kuna mtazamo wa jumla miongoni mwa wananchi kuwa usalama nchini umeimarika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kama inavyooneshwa na zaidi ya nusu ya wananchi hao  huku asilimia 37 ya watanzania wakisema hali ya usalama imebaki pale pale.
Amebainisha kwamba takwimu za sauti ya wananchi za mwaka 2015 zilionesha asilimia 57 ya wananchi hawakuwahi kuhisi hawako salama kutembea kwenye maeneo wanayoishi, lakini mwaka 2017 idadi imeongezeka kufikia asilimia 71.

Amesema  mwaka uliopita asilimia 29 ya wananchi hawakujisikia salama kutembea kwenye maeneo wanayoishi au waliogopa kufanyiwa uhalifu kwenye nyumba zao huku asilimia 16 walikiri kukaa majumbani mwao na kuwa na hofu ya uhalifu.

Aidha, amesema kwa mujibu wa utafiti huo, wananchi wameonyesha kuwa na imani kubwa na jeshi la polisi kuliko sungu sungu, walio wengi wanashindwa kutoa taarifa za uhalifu kwa jeshi hilo kutokana na kwamba vituo viko mbali.

Na Abraham Ntambara

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search