CCM yashangilia marudio ya uchaguzi wa ubunge Longido...#share

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeipongeza Mahakama ya Rufaa nchini kwa kutengua matokeo ya Uchaguzi wa Ubunge wa Jimbo la Longido mkoani Arusha yaliyompa ushindi  mgombea wa Chadema, Onesmo Ole Nangole.


Hayo yamebainishwa jana na  Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema katika uchaguzi wa jimbo hilo wa mwaka 2015, CCM ilifanya kampeni zilizozingatia misingi ya utu na ustaarabu na kudai wapinzani walitumia lugha ya kibaguzi na matusi, kusababisha chama hicho kukata rufaa katika Mahakama Kuu kanda ya Arusha.

''CCM ilifanya kampeni za utu na ustaarabu lakini mgombea mwingine alitumia lugha zinazokiuka misingi ya haki ndio maana tulienda mahakamani tukiamini haki itatendeka,'' alisema Polepole.

Amebainisha kuwa baada ya mahakama hiyo kutoa uamuzi huo, Chadema kilikata rufaa ambayo ilikataliwa kutokana na mapungufu ya kisheria, kukata upya huku rufaa hiyo ikitupiliwa mbali.

Amesema  chama hicho kinaiomba mahakama kuendelea kutimiza majukumu yake bila kuingiliwa na mhimili wowote wa Dola.

Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Steven Lemomo Kisurwa amesema katika rufaa ya kwanza mahakama ilibaini uchaguzi huo haukuwa wa haki na kuamuru urudiwe huku akibainisha endapo atachaguliwa  atazifanyia kazi kero za elimu, maji na wafugaji.

Amesema katika kipindi cha miaka miwili alijitahidi kuwatuliza wananchi wasifanye vurugu huku akisisitiza kuwa ana imani CCM kitaibuka na ushindi.

 Na Hussein Ndubikile


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search