Gumzo: "Vijana wengi wa Kitanzania wamepata ujuzi, lakini wamekosa sifa za kuajiriwa.." ILO & VETA wametuletea course ya Uanagenzi.. #share

SHIRIKA la Kazi Duniani (ILO) limesema vijana wanaohitimu Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi na Vyuo Vikuu nchini wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira kutokana kukosa sifa zinazohitajika kwenye soko la ajira.

Aidha, limebainisha katika kukabiliana na changamoto hiyo limeanzisha Mradi wa Uanagenzi wenye lengo la kuwasaidia vijana wenye ujuzi ambao hawakupata fursa ya kupata elimu kwa kuwapeleka Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini (VETA) na Chuo cha Taifa cha Utalii ili waajiriwe katika sekta hizo.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Ofisa Miradi na Uendelezaji wa shirika hilo Komoro Mwenda wakati akiwasilisha mada katika Siku ya Pili ya Mkutano wa Kitaifa wa Vijana wa Afya na Maendeleo.

Amesema kumekuwapo na kundi kubwa la vijana linalohitimu katika taasisi hizo huku akikisisisitiza kwa kiasi kikubwa ujuzi wanaopewa haukidhi sifa wanazohitaji waajiri kusababisha ugumu wa upatikanaji ajira.

“ Ngazi ya vyuo vya ufundi na vyuo vikuu kuna idadi kubwa ya vijana wamehitimu wana sifa lakini wanashindwa kuendana na mahitaji ya soko ya ajira ndio maana wengi wao wanakosa ajira,” alisema Mwenda.

 Mwenda amesema tayari ILO kwa kushirikiana na Serikali limeanza kuwapeleka vijana kwenye vyuo hivyo kuwaongezea ujuzi na kuwasaidia kutambulika kwenye fursa za ajira.

Amesesma mradi  huo umelenga kuwasaidia vijana wenye ujuzi wasiokuwa na vyeti vya taaluma waliohtimu elimu ya darasa la saba na Kidato cha nne waliopata alama D katika masomo yao.

Ameongeza kuwa tatizo la ajira kwa vijana huwasabishia msongo wa mawazo ambao huchangia kujiingiza katika matendo maovu yanayopoteza nguvu kazi ya kazi ya taifa.
Kwa upande wa Makamu wa Rais wa Shirika la Kimataifa la Save the Children Robert Clay amesema makundi ya vijana yanakabiliwa na changamoto ya upangaji wa mipango kazi wa miradi ya maendeleo inayowahusu huku akiwataka kuongeza jitihada kufanikisha hilo.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Ukimwi nchini (TACAIDS), Jumanne Issango amesema utandawazi huchangia mmomonyoko wa maadili sababu ya vijana kushindwa kuamua mambo wanaotakiwa kuyafuata na wasiotakiwa kuyaiga.

Mwakilishi Mkazi wa Masuala ya Uzazi na Uzazi wa Mpango nchini, Lulu Mwanakilala ameitaka jamii kuendelea kutumia njia za uzazi wa mpango na kwamba kabla muhusika hajaanza kutumia huambiwa madhara ya njia hizo na wataalamu.


Na Hussein Ndubikile

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search