GUMZO: Wabunge Wapya CUF 'wanasonga mbele' Madiwani nao.. 'wanasonga mbele',.. nikwambie kitu gani kingine..! and 'ze embattled CUF' 'itasonga mbele' mpaka kieleweke.. #share

Wabunge wanane wa Viti Maalum waliovuliwa uanachama na Chama cha Wananchi (CUF), na hivyo kupoteza nyadhifa zao hizo, wamegonga ukuta mahakamani, katika maombi yao ya zuio la kuapishwa kwa wabunge wapya waliochukua nafasi zao.

Wabunge hao pamoja na madiwani wawili pia wa viti maalum walikuwa wakiiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Sa laam kutoa amri ya zuio la muda dhidi ya Bunge kutokuwaapisha wabunge wapya walioteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), badala yao.


Pia walikuwa wakiiomba mahakama hiyo itoe amri ya zuio la muda dhidi ya Wakurugenzi wa Manispaa za Ubungo na Temeke, kutokuwateua madiwani wengine badala yao na kuwaapisha, kusubiri kumalizika kwa kesi yao ya msingi, waliyoifungua wakipinga kuvuliwa uanachama.

Hata hivyo harakati zao hizo hazikuzaa matunda baada ya mahakama hiyo kuyatupilia mbali maombi hayo kutokana na pingamizi la awali lilowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kulizuia Bunge katika utekelezaji wa majukumu yake.
AG alikuwa akiwawakilisha Mkurugenzi wa Uchaguzi, wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Katibu wa Bunge na wakurugenzi wa manispaa hizo.

Katika uamuzi huo Mahakama Kuu imehitimisha rasmi kitendawili cha ama kuapishwa au kutokuapishwa kwa wabunge, hadi kesi ya msingi iliyofunguliwa na wabunge hao waliovuliwa ubunge, na kwa hali hiyo wabunge hao wateuliwa wako huru kuapishwa.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Lugano Mwandambo alisema kuwa anakubaliana na hoja zilizotolewa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Haruni Matagane kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kulizuia Bunge kwa kuwa hilo ni kujumu lake la kikatiba.

Jaji Mwandambo alisema kuwa anakubaliana na hoja za Wakili Matagane kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 4 (1) ya Katiba ya Nchi, kuhusu mgawanyo wa madara kwamba kila mhimili huko huru kutekeleza majukumu yake bila kuingiliwa na mhimili mwingine, kama haukuvuka mipaka ya mamlaka yake.

Alisema kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 68 ya Katiba ya Nchi, Bunge kuwaapisha wabunge ni moja ya majukumu yake ya kikatiba na kwamba kwa hali hiyo Mahakama haina mamlaka ya kuliingilia.

AG katika pingamizi lake alikuwa amewasilisha hoja mbili za pingami. Mbali na hoja hiyo ya mamlaka ya bunge, hoja nyingine ilikuwa ni kwamba kifungu kilichotumika kufungua maombi hayo hakikuwa kifungu sahihi kinachoiwezesha mahakama kuyasikiliza.

Hata hivyo Jaji Mwandambo alitupilia mbali hoja ya kifungu hicho cha 95 cha Sheria ya Mwenendo wa Masahauri ya Madai, kuwa si sahihi, baada ya kukubaliana na hoja za wakili wa wabunge hao watoa maombi, Peter Kibatala kuwa kifungu hicho ni sahihi.

Hata hivyo, Jaji Mwandambo alifafanua kuwa kukubaliana na hoja ya AG kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kulizuia bunge kuwaapisha wabunge hao wateule hakumaanishi kuwa maombi yote ya wabunge waliovuliwa uanachama yametupiliwa mbali, isipokuwa hoja hiyo tu ya kuzuia kuapishwa kwa wabunge wateule.

Hivyo maombi hayo yatasikilizwa Jumatatu kuhusiana nafuu nyingine zinazoombwa ikiwemo ya madiwani wawili waliovuliwa uanachama nafasi zao kutokutangazwa kuwa ziko wazi, kuteuliwa wengine badala yao wala kuwaapisha.


Wajibu maombi wengine walikuwa ni Bodi ya Wadhamini wa CUF, Mwenyekiti wa Taifa na Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, ambao pia walitoa taarifa ya pingamiz la awali lakini wakati wa usikilizwaji, hawakuweza kuwasilisha hoja zao na hivyo mahakama haikuzingia sababu zao za mapingamizi.

James Magai,

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search