Mbarawa aitaka NCC kuwa chachu ya maboresho ya sekta ya ujenzi nchini..
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amelitaka Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), kuja na mapendekezo ambayo yataboresha sekta ya ujenzi nchini ili iweze kuchangia pato la Taifa kwa kiwango kikubwa na kuchochea uchumi wa nchi.
Aidha, amelitaka baraza hilo kuhakikisha linakuja na utaratibu ambao utasaidia uwepo wa bei moja katika ujenzi ili kuondoa mkanganyiko wa kila mkandarasi kujenga kwa gharama anazotaka.
Profesa Mbarawa aliyasema hayo wakati akifungua semina kwa wadau wa ujenzi ambao wamekutana kwa siku moja jijini Dar es Salaam kujadili ripoti ya wataalam washauri ambao wameikusanya kuhusu sekta hiyo.
Alisema sekta ya ujenzi ni sekta muhimu katika ujenzi wa uchumi viwanda kama matarajio ya Rais John Magufuli katika kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati hivyo NCC inatakiwa kubadilika na kuendana na dhana hiyo.
Waziri Mbarawa alisema kwa mujibu wa taarifa za mwaka jana sekta hiyo imechangia asilimia 14 ya pato la Taifa hivyo jitihada zinahitajika zaidi ili kuongeza asilimia hiyo.
Alisema wadau wa sekta hiyo wanapaswa kuja na mapendekezo ya nini kifanyike ili kuboresha sekta hiyo hivyo basi semina hiyo iwe ni sehemu sahihi kupitia ripoti ya wataalam na kuja na majibu sahihi.
Mbarawa alisema Serikali ipo tayari kupeleka mapendekezo ya mabadiliko ya sheria kama wadau watahitaji hivyo kuwataka wawe huru kutoa maoni ya mini kifanyike kwa maslahi ya nchi.
"Sisi tunasubiri mapendekezo yenu mkitaka tubadilishe sheria au kanuni tupo tayari kwa maslahi ya nchi na wananchi kwani sekta hii ni muhimu kwa maendeleo kutokana na kugusa kila sekta," alisema.
Alisema ni jukumu la kila mdau na mtaalam kutembea na dhamira ya nchi hivyo ni matarajio yake kuwa wadau hao watatoka na mapendekezo sahihi kwa maslahi ya nchi.
Akizungumzia kuhusu kuwepo na usawa wa gharama za kulipia mita moja ya ujenzi wa nyumba, barabara, viwanja vya ndege na kwingine alisema angependa wadau hao wanatoa mapendekezo kwa NCC ili iweze kutoa bei elekezi.
Alisema katika hali ya kusikitisha leo hii mtu akitaka kujenga hajui gharama sahihi ya kujenga mita moja hali ambayo inachangia kila mjenzi kuwa na gharama zake.
"Ukiniuliza hapa bei ya kujenga mita moja ya nyumba, barabara, kiwanja cha ndege sijui lakini NCC wapo nadhani mnapaswa kuliangalia hili kwa jicho la kipekee ili kuondoa udanganyifu," alisema.
Waziri alisema ni wazi kuwa gharama zinaweza kutofautiana kulingana na nyakati hasa thamani ya fedha kushuka na kupanda lakini itakuwa jambo jema kama kama bei itajulikana awali kuliko ilivyo sasa.
Kwa upande wake Mwnyekiti wa NCC Profesa Mayunga Mkunya alisema baraza limejipanga kuendana na kadi ya Serikali hivyo kumuahidi Waziri Mbarawa kuwa watatekeleza yote ambayo serikali inataka.
Profesa Mkunya alisema semina hiyo ya wadau itakuja na majibu sahihi ya nini kifanyike kutokana na mependekezo ya wataalam washauri ambao waliongozawa na Mhandisi Dk. Ramadhan Mlinga ili kuweza kusaidia sekta hiyo.
"NCC imejipanga kusimamia sekta hii kwa nguvu zote kuanzia ubora wa ujenzi na yote ambayo yanahusu sekta hii ili kuchochea ukuaji wa uchumi," alisema.
Katibu Mkuu Wizara hiyo sekta Ujenzi, Mhandisi Joseph Nyamuhanga alisema kamati hiyo imepitia sheria iliyopo, maboresho ya baraza njia mbadala.
No comments:
Post a Comment