Askari polisi 7 kikaangoni kwa udhalilishaji, uharibifu..Soma habari kamili na Matukio360..#share

Na Hussein Ndubikile

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imetoa pendekezo kwa Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polis IGP, Simon Sirro kuwachukulia hatua za kinidhmu askari saba walioshiriki tukio la ukamataji Oktoba 10,2017 katika kiwanda cha Juisi aina ya Sophy kilichopo wilayani Mkuranga mkoani Pwani kwa kosa la udharirishaji na uharibifu wa mali.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Bahame Nyanduga akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam

Askari hao ni Salehe Abdallah,  G5941 PC Nuhu, E.9972 D/Cpl Trano,  A/Inspekta Janeth, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jafari Ibrahim, aliyekuwa OCD wa Mkuranga, Edson Kasekwa mwaka 2016 na aliyekuwa OCD wa Mkuranga mwaka 2015  Mayenga Mpalala.

Walalamikaji ni Jimmy Sandy, Gandi Tengeza na John Wagesa.

Mapendekezo hayo yametolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa tume hiyo, Bahame Nyanduga wakati akisoma Muhtasari wa Uamuzi wa Tume katika Shauri namba HB/00674/15/16/polisi/Pwani.

Amesema tume hiyo ilipokea lalamiko la Sandy Julai 15 mwaka jana akiwalalamikia askari waliotajwa kumdhalilisha kwa kumpiga mke wake, Gandi na watoto wake pamoja na wafanyakazi wake wa kiwanda hicho huku akiongeza baadhi ya askari hao  waliharibu mali mali na kupora Sh 16,500,000.

“ Mlalamikaji namba 1 na 2 walidai kuwa katika siku mbili tofauti yaani Juni 6  na 8 mwaka huu, mlalamikiwa wa 5 na 8 na kumtaka mlalamikaji wa kwanza atoe rushwa ya Sh 200,000 kutokana na maagizo ya mlalamikiwa wa 3 aliyekuwa RPC wa Pwani na aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mkuranga,” amesesma.

Amebainisha kuwa Jeshi hilo mkoani humo limfungulie mashitaka Afisa Chakula ma Madawa wa wilaya hiyo, Elinas Nko kwa kosa la kudharau amri tume hiyo.

Amependekeza kuwa jeshi la polisi liboreshe miundo mbinu ya Kituo cha Polisi cha Mkuranga kwa kujenga mahabusu ya wanawake pamoja na kuandaa program itakayowapatia mafunzo ya kuwakumbusha askari polisi waliopo kazini masula ya haki za binadamu mara kwa mara.

Amesisitiza kuwa jeshi hilo liwarudishie mlalamikaji namba 1 na 2 fedha  na mali zilizokamatwa katika kiwanda hicho.

Pia amependekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza tuhuma za rushwa za askari waliotajwa na walalamikiwa waliofanyiwa vitendo vya uvunjivu wa haki za binanadamu.
Nyanduga ametoa pendekezo kwa mlalamikaji namba 1 na 2 kuhakikisha kuwa kabla ya kuanza biashara yeyote wanatakiwa kufuata taratibu na sheria zinazoongoza uzalishaji wa bidhaa.

Katika hatua nyingine, amesema tume hiyo imemshukuru mlalamikiwa wa kwanza Kamanda wa Mkoa wa Pwani, Bonaventure Mushongi kwa kuwajibika mbele ya THBUB ingawa hakuwa kamanda wa mkoa wakati wa oparesheni ya uvamizi na kwamba amefanikisha kujulikana kwa wahusika wa tukio hilo.

Aidha, amesema mapendekezo hayo yaliyoelekezwa kwa mamlaka zote  yanatakiwa kutolewa taarifa ya utekelezaji ndani ya siku 90 kwa tume hiyo kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 28(2) cha sheria ya tume na 7./2001 sura ya 391 ya Sheria za Tanzania.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search