Vigogo uhujumu uchumi walia njaa Mahakamani...soma habari kamili na Matukio360
Na mwandishi wetu
Mkurugenzi wa Tathmini, Archard Alphonce Kalugendo
(49) na Mthamini wa Madini ya Almas wa Serikali, Edward Joseph Rweyemamu (50)
wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iwasaidie kuzipata
kadi zao za Benki ambazo walinyang'anywa wakati walipokamatwa.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
Washtakiwa hao wametoa ombi hilo leo mbele ya Hakimu
Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage wakati kesi hiyo ilipotajwa na wanaomba
kurejeshewa kadi zao za Benki kwa sababu wanafamilia na mishahara yao inapitia
huko, wasaidiwe kuzipata ili wasaidie familia zao.
Kufuatia ombi hilo, Hakimu Mwijage alimtaka Wakili wa
Serikali, Simon Wankyo na wakili wa washtakiwa Nehemia Nkoko walifanyie kazi
hilo ili familia za washtakiwa hao zisije kufa kwa njaa na kesi hiyo
itakapotajwa wapeleke taarifa.
Awali, Wakili wa Serikali, Wankyo amedai jalada la kesi hiyo ya uhujumu uchumi linapangwa kwa ajili ya kupelekwa kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na kuna maeneo machache walikuwa wakiyafanyia kazi.
Hata hivyo amedai tarehe ijayo wataeleza ni hatua ipi waliyoifikia na akaomba ipangiwe
tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Wakili wa washtakiwa hao, Nehemiah Nkoko ameiambia
Mahakama kuwa taarifa hiyo iliyotolewa na upande wa Mashtaka ni hatua nzuri na
akaomba juhudi zifanyike katika upangaji wa hilo jalada.
Kesi hiyo imehahirishwa hadi Novemba 9,2017. Washtakiwa hao wanakabiliwa
na kesi ya uhujumu uchumi kwa
kusababisha hasara ya dola za Kimarekani 1,118,291.43 sawa na Tsh
2,486,397,982.54.
Kalugendo ambaye ni Mkazi wa Kinyerezi na Rweyemamu
Mkazi wa Mwananyamala wote ni waajiriwa wa Wizara ya Nishati na Madini.
Kati ya Agosti 25 na ,31, 2017 katika maeneo
mbalimbali kati ya Dar es Salaam na Shinyanga, washtakiwa hao kwa pamoja na kwa
vitendo vyao wakiwa wathamini walioajiliwa na Wizara ya Nishati na Madini
walisababisha hasara ya kiasi hicho cha fedha.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa hao
hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya
kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu. Washtakiwa wapo rumande.
No comments:
Post a Comment