Waziri Lukuvi apiga 'Stop' bomoa bomoa kwa waliojenga bila vibali...Soma habari kamili na Matukio360..#share

Na Abraham Ntambara

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewataka Maofisa Mipango Miji kutowasumbua kwa kuwabomolea nyumba  wananchi waliojenga katika viwanja vyao bila kuwa na vibali.
Waziri wa Ardhi, Nyomba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Nne wa Bodi ya Wataalamu wa Mipangomiji jijini Dar es Salaam.

Pia ameitaka Bodi ya Wataalamu wa Mipangomiji kuandaa miongozo rahisi ya mipango miji itakayotumika na watendaji wa serikali za mitaa na vijiji ili kuepusha migogoro mbalimbali ya ardhi nchini.

Kauli hiyo ya Waziri Lukuvu ameitoa leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Nne wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji, amesema ujenzi bila vibali ni tatizo lililosababishwa na baadhi ya watendaji wa idara ya ardhi ambao walishindwa kusimamia vyema mfumo huo.

"Kwa sasa hakuna kumsumbua mtu yeyote aliyejenga katika eneo lake halali bila vibali, hii ni kwa sababu serikali yenyewe kupitia watendaji wake walishindwa kusimamia vizuri, lakini kinachotakiwa pia kwa wale waliojenga makazi holela wanatakiwa kupimiwa na kurasimishwa ardhi," amesema Lukuvi.

Amesema kwanzia sasa ni marufuku kwa Maofisa wa Mipango Miji kuwasumbua wananchi hao, isipokuwa wale waliojenga makazi holela wanatakiwa kupimiwa na kurasimishwa maeneo yao ili waweze kuyamiliki kihalali kwa mujibu wa sharia.

Akizungumzia kuhusu kukosekana kwa miongozo rahisi katika ngazi za mitaa na vijiji, amesema inachangia kuwepo kwa mipango miji mibovu na kuongeza kuwa miongozo hiyo itasaidia watendaji wa mitaa na vijiji kusiamia zoezi la upangaji wa miji ambalo linanafanyika ndani ya miaka 10 kwa nchi nzima.

Ameongeza kuwa serikali imeamua kuzipa kipaumbele Kampuni za ndani katika kusimamia zoezi la upangaji miji kutokana na kwamba zimekuwa zikifanya kazi nzuri na kwa gharama ya chini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo Profesa Wilbard Kombe amesema tasnia ya mipangomiji bado ni changa kwa maana kwamba wataalam wa mipanomiji  ni wachache ukilinganisha na mahitaji.

“Tafiti zinaonyesha kuwa wataalamu waliopo ni asilimia 25 tu ya mahitaji. Pamoja na hayo, kati ya wataalamu takribani 700 wenye taaluma ya mipangomiji ni wataalamu 306 tu waliosajiliwa hadi sasa,” amesema Prof. Kombe.

Aidha ameongeza kuwa zipo mamlaka za upangaji ambazo haziajiri wataalamu wa Mipangomiji na kupelekea baadhi ya Halmashauri kukosa wataalamu hao, huku Sheria ya Mipangomiji No 8 ya mwaka 2017 ikizitaka Halmashauri zote kuwa na wataalamu wa Mipangomiji aliyesajiliwa na bodi.

Ameomba Halmashauri zote nchini kuhakikisha zianaajiri wataalamu wa mipangomiji waliosajiliwa au kuhimiza waliopo kusajiliwa kama wanazo sifa za kusajiliwa.






About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search