Waziri Jafo awapa mtihani wakuu wa mikoa...Soma habari kamili na Matukio...#share
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo ameagiza
kila mkuu wa mkoa nchini kuhakikisha anajenga viwanda vipya 100 katika kipindi
cha mwaka mmoja kinachoanzia Desemba 2017.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo
Kauli hiyo ameitoa leo wakati akizungumza na wakuu wa mikoa
wapya walioapishwa juzi na Rais John Magufuli, Jafo amewataka kuitekeleza sera
ya ujenzi wa viwanda ipasavyo.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo Desemba 2018
kila mkoa uwe umejenga viwanda vidogo na vya kati visivyopungua 100, mikoa 26
ya Tanzania Bara inatakiwa kuwa na viwanda vipya vidogo na vya kati
visivyopungua 2,600 ifikapo Desemba 2018,” amesema Jafo.
Aidha amesema Serikali imekusudia kufikia nchi ya uchumi wa
kati kupitia ujenzi wa viwanda huku akiwataka wakuu hao kuibua viwanda vidogo
na vya kati kwa kuhamasisha ushiriki wa viongozi ndani ya mikoa na wananchi
katika maeneo yao ya utawala.
Jafo ameongeza kuwa, katika kusimamia utekelezaji wa agizo
hilo ofisi yake itaweka utaratibu maalumu wa kupima utendaji kazi wa kila
kiongozi wa mkoa kwa kuangalia ushiriki wake wa kuwajengea hamasa viongozi wa
chini wakiwamo wakuu wa wilaya na wananchi.
Ameeza katika kufanikisha dhana ya ujenzi wa uchumi wa
viwanda, Serikali inaendelea kuweka mkazo na kipaumbele katika upatikanaji wa
malighafi za kilimo na kuwataka wakuu wa mikoa kuhakikisha kuwa maofisa ugani
wanatekeleza vyema majukumu yao ya kazi.
Kwa upande mwingien Waziri Jafo amewataka wakuu hao wa mikoa
kusimamia makusanyo ya fedha za ndani katika halmashauri na kutumia vyema
asilimia tano zinazotengwa kuwawezesha wananchi kupata mikopo ili washiriki
katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema ili
kufanikisha dhana ya uchumi wa viwanda, Serikali haina budi kuwapa msukumo na
ushirikiano wa karibu wanasayansi utakaowezesha kuibua viwanda vingi zaidi
pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za kilimo nchini.
Mbali na Malima, wakuu wengine wa mikoa waliohudhuria mkutano
huo ni Robert Luhumbi (Geita), Joachim Wangabo (Rukwa), Galesius Byakanwa
(Mtwara) na Christine Mndeme (Ruvuma).
No comments:
Post a Comment