Kampuni 500 kushiriki maonesho nchini...soma habari kamili na matukio360..#share
Na Abraham Ntambara
ZAIDI ya kampuni 500 yanatarajia kushiriki katika maonesho ya
pili ya bidhaa za viwanda yatakayofanyika
kuanzia Desemba 7 hadi 11, 2017 katika uwanja wa maonesho wa mwalimu J.K
Nyerere.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage akizungumza na waandishi wahabari jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam juu
ya maandalizi ya maonesho hayo, Waziri wa Viwanda na Biashara Charles Mwijage
amesema katika maonyesho ya mwaka jana ni makampuni 472 pekee ndiyo
yaliyoshiriki.
“Lengo kuu la maonesho haya ni kujenga jukwaa kwa wadau wa
viwanda kupata fursa ya kujadiliana, kubadilisha uzoefu na kutangaza biashara
za watanzania wote wanaomiliki viwanda vidogo, vya kati na vikubwa,” amesema
Mwijage.
Mwijage amesema maonesho hayo mwaka huu yanabeba kauli mbiu
isemayo “Tanzania sasa tunajenga viwanda” ikilenga kuwaaminisha wananchi juu ya
falsafa na dhima ya ujenzi wa viwanda wa uchumi wa viwanda.
Ameongeza, meonesho hayo yatawakutanisha wadau wa viwanda
ikiwemo wazalishaji wa malighafi, taasisi zinazotoa huduma mbalimbali kwa wenye
viwanda na taasisi zinazowezesha wenye bidhaa kutoka kiwandani mpaka kufikia
kwa mtumiaji.
Amesema wakati wa maonesho Desemba 11, 2017 itakuwa siku
maalumu ya viwada Afrika ambayo itaratibiwa na kwa ushirikiano na Taasisi za
Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Viwanda (UNIDO).
Waziri Mwijage amesema wizara yake kupitia Mamlka ya
Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan Trade) imewakaribisha watanzania
wanaomiliki viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kushiriki maonesho hayo.




No comments:
Post a Comment