Kitilya wenzake waendelea kusota rumande....soma habari kamili na matukio360....#share


 Na Abdulrahim Sadiki, Dar es salaam 

UPELELEZI katika kesi inayomkabili  Mwenyekiti wa Kampuni inayoshughulikia  uwekezaji wa mitaji na dhamana (Egma), Harry Msamire Kitilya na waliokuwa maofisa wa benki ya Stanbic, Shose Mori Sinare na Sioi Graham Solomon bado haujakamilika.


Kitilya na wenzake wakiwa katika moja ya chumba cha mahakama ya hakimu mkazi Kisutu.

Hayo yamesemwa leo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.

Kishenyi amedai viongozi wa Mashtaka na Uchunguzi wanafanya jitihada za kukamilisha upelelezi na kwamba muda si mrefu utakamilika.

Wakili wa washtakiwa, Alex Mgongolwa ameutaka upande wa mashtaka kuharakisha  upelelezi.

Baada ya kutolewa kwa hoja hizo,Hakimu Nongwa ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 16, 2018 kwa ajili ya kutajwa na kuutaka upande wa mashtaka kufanya linalowezekana upelelezi ukamilike.

Awamu ya kwanza ya vielelezo hivyo  kutoka nchini Uingereza ilikwisha pokelewa  bado wanasubiri awamu ya pili.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa dola za Marekani 550 milioni  kwa  serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard Uingereza.

Wanadaiwa kuwa  Machi 2013 jijini Dar es Salaam walijipatia Dola za Marekani 6 milioni, wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji upatikanaji wa mkopo  na zililipwa kupitia  Kampuni ya Egma T Ltd.

Washtakiwa  hao wanadaiwa  kutakatisha fedha kwa kuhamisha, kuchukua na kuweka kiasi cha Dola za Marekani 6 milioni katika akaunti tofauti tofauti  za benki.

Kati ya  Machi 2013 na Septemba 2015, wanadaiwa  kuwa waliweka pesa hizo katika akaunti mbalimbali zilizomilikiwa na kampuni ya Egma na kwamba walipaswa kufahamu kuwa pesa hizo ni mazao ya uhalifu wa kughushi. 



About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search