Mahakama yaelezwa afya ya Rugemarila, Harbinder Sethi ni 'tete'....soma habari kamili na matukio360....#share
Na Abdulrahim Sadiki, Dar es salaam
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imeelezwa kuwa afya ya mmiliki wa IPTL, Harbinder Singh Sethi na mfanyabiashara, James Rugemarila zinaendelea kuzohofika na ni za mashaka.
Rugemarila na Herbinder Sethi wakiwa katika mahakama ya Kisutu
Hayo yameelezwa na Wakili wa utetezi, Respicius Didas baada ya Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leornad Swai kumueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Swai amedai kuwa anaomba kesi hiyo iahirishwe hadi tarehe nyingine, pia walienda Magereza kuchukua maelezo ya Seth lakini ilishindika kwa sababu afya yake haikuwa nzuri.
Baada ya kueleza hayo, Wakili Didas amedai kuwa wakati afya za washtakiwa zikiendelea kuwa za mashaka wanauomba upande wa mashtaka ukamilishe upelelezi.
"Ni rai yetu kwamba kila kesi hii inapoahirishwa baada ya siku 14 kuwe na kitu kipya kuhusu hatua zilizochukuliwa, lakini inavyoonekana upande wa mashtaka unachukulia kawaida kuahirishwa kwa kesi,".
Pia alidai kuwa upande wa mashtaka unacheza na mamlaka, utambue hali za washtakiwa ni mbaya, hivyo ukamilishe upelelezi.
Wakili Swai alidai kuwa serikali inajitahidi kuangalia afya za washtakiwa kwani hata mara ya mwisho serikali ilizungumzia afya ya Seth ambaye alidai anataka madaktari wake wawepo wakati akifanyiwa upasuaji.
Kuhusu upelelezi, Swai amedai kuwa ni kweli unachukua muda mrefu ila upo katika hatua za mwisho na kitu kinachochelewesha ni upelelezi mwingine kuwa nje ya nchi.
" Mchakato wa upelelezi wa nje ya nchi(Malaysia) una process, lakini serikali inajitahidi,"alidai Swai.
Hata hivyo, Rugemarila aliieleza Mahakama kuwa hajawahi kupelekwa Hospital ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu, pia anahisi ana kansa.
"Ninafahamu nina kansa kwa sababu ya huu uvimbe nilionao, pia Swai amesema daktari wangu kasema sina kansa na bahati amefiwa angekuja Mahakamani kusema kwamba nina kansa".
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Shaidi amesema mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa amri wakatibiwe nje ya nchi na alishatoa amri kwamba watibiwe Muhimbili na kama inahitajika wakatibiwe nje ya nchi serikali ndio itasimamia. Ameahirisha kesi hadi Februari 16,2018.
Kwa pamoja washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh.Bil 309.
About Author Matukio360
Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.
No comments:
Post a Comment