ACT Wazalendo wafungua kesi madai dhidi ya jeshi la polisi.... soma habari kamili na matukio360...#share
Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam
CHAMA cha ACT-Wazalendo kimefungua kesi ya madai Na. 8/2018 mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam kulishtaki jeshi la polisi ikidai jeshi hilo kuingilia visivyo halali shughuli za ziara za viongozi wa chama hicho kwenye kata wanazoongoza.
Pia kimejipanga kupeleka bungeni mpango mbadala juu ya sera za kibajeti za nchi kwa kupinga mpango wa sasa wa bajeti unaojikita kwenye maendeleo ya vitu badala ya maendeleo ya watu.
Zitto Kabwe akizungumza na waandishi wa habari
Hayo yemesemwa leo jijini Dar es Salaam na kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelezea waliyobaini katika ziara za viongozi walizofanya katika kata wanazoongoza kuanzia Febriari 19, 2018 hadi Machi 13, 2018.
“Ziara yetu kwenye kata tunazoongoza ilibughudhiwa na vyombo vya dola. Jeshi la polisi na baadhi ya watendaji wa serikali walihaha sana kuingilia na kujaribu kuikwamisha ziara yetu,” amesema Zitto.
Ameongeza “Kilele cha jitihada hizi ni kukamatwa na kulazwa kwangu rumande Mkoani Morogoro usiku wa kuamkia Februari 23, 2018 nikiwa katika kata ya Kikeo, Mvomero, Morogoro, kuzuiliwa kutembelea miradi ya maendeleo kwenye kata za Vumilia-Urambo na Usinge-Kaliua mkoani Tabora pamoja na kuzuiwa kabisa hata kufanya mkutano wa ndani na diwani wetu katika kata ya Liale, Mvomero, mkoani Morogoro.”
Akizungumzia kuhusu kupeleka bungeni mpango mbadala juu ya sera za kibajeti, Zitto amesema masuala watakayosimamia ni uchumi shirikishi unaozalisha ajira kwa kuhakikisha kilimo pamoja na viwanda vinavyoongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo ndio kipaumbele kikuu, usalama wa chakula na lishe, pamoja na huduma bora za kijamii, hasa maji, elimu na Afya.
Waliyobaini katika ziara
Kiongozi huyo ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini, amesema katika ziara hiyo imewaonyesha kuwa hali ya maisha ya wananchi vijijini ni mbaya sana.
Amesema katika kata zote walizotembelea wamekuta tatizo kubwa ni hali mbaya ya kipato, migogoro ya ardhi, kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama, ukosefu wa huduma bora za afya, tatizo la miundombinu ya usafirishaji, ukosefu wa pembejeo za kilimo na ukosefu wa masoko ya mazao ya wavuvi, wakulima na wafugaji pamoja na kushuka kwa bei ya mazao yao.
Mengine ni kupanda kwa gharama ya maisha ya watu, kupanda kwa gharama ya vifaa vya ujenzi, upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, vyoo pamoja walimu na kuzorota kwa hali ya usalama wa wananchi pamoja mali zao, hali mbaya ya ajira kwa vijana pamoja na uminywaji mkubwa demokrasia na uhuru wa vyobo vya habari.
Pia Zitto ameendelea kuweka msisitizo uwepo wa mkutano wa maridhiano wa kuona ni namna gani shughuli za kisiasa zinaweza kufanyika nchini kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
About Author Matukio360
Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.
No comments:
Post a Comment