Kesi ya uchochezi ya Tundu Lissu yaunguruma mahakamani... soma habari kamili na matukio360...#share


Na Abdulrahim Sadiki,Dar es salaam

KESI ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singinda Mashariki( Chadema),Tundu Lissu na wahariri wa gazeti la Mawio  imeendelea leo  katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es salaam


Wakili wa Serikali, Patrick Mwita ameeleza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba kuwa mshitakiwa wanne anayekabiliwa na kesi hiyo ambaye ni Lissu anaumwa yupo nje ya nchi kwa matibabu.

Hata hivyo, Wakili Mwita aliieleza mahakama kuwa Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi anafanya Mawasiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili kuona njia nzuri ya kuendelea na kesi hiyo.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo,Hakimu Simba ameiahirisha kesi hadi Aprili 30,2018 Kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa wengine  katika kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina, Jabir Idrisa na  Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa Januari 12 hadi 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, washtakiwa watatu, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa‎ za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam,  walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob  anadaiwa kuwa Januari 13,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala,  Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokua na taarifa za uchochezi.

Mshtakiwa huyo pia  anadaiwa kuwa alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya  sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Mbali na mashtaka hayo washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016,  Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka yoyote, waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar   wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search