Waziri Mwijage atoa ya moyoni...Soma habari kamili na Matukio360..#share

Na Salha Mohamed

WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amewataka wafanyakazi nchini kutong'ang'ania kuajiriwa kwenye viwanda wasivyokuwa na maslahi na badala yake wafungue viwanda vidogo vya kuchakata malighafi na kuajiri watu wengi.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.

Hayo yamebainishwa Dar es Salaam leo, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu Afrika yenye kauli mbiu 'Uchumi wa Viwanda na Haki za Wafanyakazi nchini' yaliyoandaliwa na Tume ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Amesema hapa nchini hakuna tatizo ya haki za binadamu hivyo wananchi wanapaswa kujenga viwanda ili kukuza uchumi wa kati hadi kufikia 2025 na kuondoa vikwazo.

"Kufanya kazi kwenye kiwanda cha mtu si ndoa katoliki kwamba haiwezi vunjika, mtoke mkafanye kwengine viwanda vingine vipo vingi hapa nchini...uzuri wa watanzania wanafundishika, utakosa kazi kiwandani kama ukienda kuomba kazi ukisema unataka kazi yeyote,"amesema Mwijage.

Amesema wafanyakazi wanapaswa kutojiingiza katika mikataba ya muda mrefu kwa kufanya hivyo ni kutawafunga kutofuata fursa kwenye viwanda vingine vyenye maslahi zaidi.

Mwijage amewataka wafanyakazi kufanya kazi kwa weledi na kuwa na ujuzi zaidi ya mmoja kwani sheria za kuwalinda zipo na wakiona zningine waseme ili waishi vizuri.

"Kazi ni nyingi, lakini watendaji kazi hawapo kama vitabu vitakatifu vilivyosema, ujenzi wa uchumi wa viwanda ni zaidi ya ujenzi wa Kiwanda vijana wawe na uthubutu na nguvu ya kutoka," amesema.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Iddi Mapuri amesema haki za wafanyakazi zinalindwa na Katiba na Sheria za nchi, wafanyakazi wanakabiliwa na changamoto za ubaguzi, mazingira duni ya kazi.

"Changamoto zingine ni kutozingatiwa kwa saa za kazi kinyume na sheria, kukosekana kwa muda wa kazi wa ziada, ujira usio stahiki, kutokuwepo kwa vyama vya wafanyakazi katika baadhi ya ajira,kutozingatiwa ipasavyo usalama wa afya kazini,"amesema.

Amesema hali hiyo husababisha wafanyakazi kuwa katika hatari ya kudhurika sehemu za kazi na kutokuwepo kwa mifumo au taratibu muafaka za ndani za kushughulikia malalamiko.
Mapuri ameongeza kuwa jitihada za ukuaji wa viwanda unaweza kuathiri haki za makundi mengine ambayo si wafanyakazi kama kuvunjwa kwa haki ya kumiliki ardhi hasa kipindi cha utwaaji ardhi kwa ajili ya miradi ya viwanda.

Amesema athari nyingine ni kukosa haki ya afya na mazingira safi na salama endapo kuna uchafuzi kutoka viwandani na madhara ya ajira kwa watoto kwani Tume imekuwa ikipokea malalamiko mengi ya uvunjwaji wa haki za binadamu mahala pa kazi.

Ameongeza kuwa Serikali kama mdau wa maendeleo ya wananchi itazingatia na kutekeleza jukumu la msingi la kulinda, kuheshimu na kuzingatia haki za binadamu pale inapotekeleza miradi mbalimbali za maendeleo.

Mkuu wa Idara ya Sheria Chama Cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara (TUICO), Noel Nchimbi amesema kumekuwa na malalamiko ya mahusiano kati ya mwajiri na mwajiriwa huku akibainisha si kila mtu anapaswa kuajiriwa.

"Ajira zipo nyingi, lakini si kila mtu anahaki ya kufanya kazi na kuajiriwa, mtoto chini ya miaka 14 hapaswi kuajiriwa kwani inaharibu afya zao hasa shuguli za migodini, mashambani na hata uvuvi ikibainika mwajiri atashitakiwa na kulipa faini ya sh milioni moja au kifungo mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.

Baadhi ya wafanyakazi hao wameitaka serikali kuangalia mazingira bora na wezeshi kwa watu wenye ulemavu huku sheria za kazi zizingatiwe kwa kila mfanyakazi.


Maadhimisho hayo yanalengo la kuikumbusha jamii umuhimu wa kukuza na kulinda haki za binadamu katika Afrika na kuongeza uelewa wa masuala ya haki za binadamu kama zinzvyotamkwa katika mkataba wa Afrika na Haki za Binadamu na Serikali wa Afrika uliopitishwa June 1981.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search