Kunguni, chawa, viroboto waibua balaa Mbarali....soma habari kamili na matukio360...#share
Na mwandishi wetu, Mbarali.
SINTOFAHAMU imeibuka kwa wakazi wa kata ya Igurusi Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya kwa kushambuliwa na viroboto, chawa na kunguni kwa njia ya kishirikina.
Pia baadhi ya wanandoa kuingia katika migogoro inayotokana na kuingiliwa kimwili kwa njia ya kishirikina.
Hata hivyo serikali mkoani humo imepiga marufuku wananchi kuchanga fedha kwa ajili ya kumwita Sangoma maarufu kama rambaramba kwa lengo la kuondoa kunguni,chawa na viroboto waliopo kwenye makazi yao kwa njia ya kishirikina.
Mkuu wa mkoa huo, Amos Makalla alipiga marufuku hiyo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Igurusi wilayani mbarali mkoani hapa baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa sangoma huyo akipiga ramli.
"Ni marufuku, Mkuu wa wilaya weka kambi katika kata hii hakikisha wanaoshawishi michango wanachukuliwa hatua sambasamba na huyo sangoma, kitendo hicho ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, serikali haiamini ushirikina na anayehitaji kufanya mambo hayo apambane na hali yake," alisema Makalla.
Mkazi wa Igurusi, Jerat Mwambusi alisema wamechoshwa na ushirikina uliopo na kuna wakati hata wanandoa wanaingia katika migogoro inayotokana kuingiliwa kimwili kwa njia za kishirikina.
Alisema wanaomba serikali kuingilia kati suala hilo kwani
wananchi hawalali usiku kucha kutokana na wadudu hao hatari kumwagwa kwenye makazi yao na licha ya kumwaga dawa wamekuwa wakiongezeka kila siku.
Neema Saimon aliitaka serikali itoe kibali kwa sangoma huyo ili aweze kuondoa wadudu hao ambao wametumwa kwa njia za kishirikina.
"Jamani kata hii inatisha kwa ushirikina kwa kweli tangu tumchukue rambaramba kwa wiki mbili tumelala salama kabisa sasa kitendo cha serikali kupiga marufuku kwa kweli tutalazimika kuhama makazi."alisema.
Mkuu wa wilaya ya mbarali, Reuben Mfune amesema utekelezaji wa agizo utafanyika na kuhakikisha waliohusika kushawishi wananchi kuchangia fedha wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
About Author Matukio360
Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.
No comments:
Post a Comment