Tanroads yatakiwa kulinda miundombinu ya barabara.... soma habari kamili na matukio360...#share

Na mwandishi wetu,
KAMATI ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Tanroads kuja na mikakati bora ya kuilinda miundombinu ya barabara za lami inazozijenga  nchini ili ziwe fursa za kiuchumi badala ya kuwa chanzo cha ajali.



Meneja wa Wakala wa Barabara( TANROADS), mkoa wa Tabora Eng. Damian Ndabalizi wa tano kushoto akifafanua jambo kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilipokagua barabara ya Manyoni-Itigi-Tabora KM 259 inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Moshi Sulemani Kakoso amesema  hayo mara baada ya kamati yake kutembelea ujenzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Tabora KM 259 inayojengwa kwa kiwango cha lami na kusisitiza kuwa umefika wakati kwa TANROADS kutoa elimu kwa jamii za vijijini kuzilinda barabara zinazojengwa na kuzitumia fursa za uwepo barabara za lami kujiletea maendeleo.

“Hakikisheni mnakuwa na programu endelevu za kuwaelimisha wananchi umuhimu wa barabara za lami ili badala ya kuzihujumu kwa kuharibu miundombinu ya barabara hizo wazilinde na kuzitumia kuibua fursa za kiuchumi na kijamii katika maeneo yao," amesema Kakoso.

Akizungumza katika ziara hiyo Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anaeshughulikia sekta ya Ujenzi, Elias John Kwandikwa ameihakikishia kamati hiyo kuwa Serikali imejipanga kuufungua mkoa wa Tabora kwa kuhakikisha unafikika kwa pande zote kwa barabara za lami.

“Tumeigawa barabara hii katika sehemu tatu ili kuharakisha ujenzi wake ambapo sehemu ya Manyoni- Itigi- Chaya KM 89.5 na Tabora–Nyahua KM 85, ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika na sehemu ya Chaya-Nyahua KM 85.4 mkandarasi anaendelea na ujenzi”, amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.

Meneja wa TANROADS mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo na Tabora Eng. Damian Ndabalinzi wameihakikishia Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuwa watatekeleza utoaji elimu ya matumizi bora ya barabara na kudhibiti maeneo yenye ajali nyingi katika mikoa yao ili jamii katika mikoa hiyo zinufaike na uwepo wa barabara za  lami.

Kamati ya Bunge ya Miundombinu iko katika ziara ya kutembelea miundombinu inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika mikoa ya Singida, Tabora na Kigoma ili kujifunza na kushauri namna bora ya kuendeleza miundombinu nchini na hivyo kuwezesha malengo ya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kutekelezeka.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search