Vigogo watano TPDC wapandishwa kortini....soma habari kamili na matukio360...#share
Na Abdulrahim Sadiki, Dar es Salaam.
Vigogo watano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la matumizi mabaya ya madaraka.
Vigogo watano wa TPDC wakifikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu leo.
Leo wakili wa Takukuru,Emmanuel Jacob amewataja washtakiwa hao kwa Hakimu Mkazi Mkuu,Wilbard Mashauri kuwa ni Mkurugenzi Mtendaji, James Mataragio.
Wengine ni, Kaimu Meneja wa uvumbuzi, George Seni, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na utawala, Wellington Hudson, Mkurugenzi wa Mkondo wa juu,Kelvin Komba na
Edwin Riwa ambaye ni kaimu Mkurugenzi wa mipango.
Akiwasomea mashtaka washtakiwa hao, Wakili Jacob amedai kati ya Aprili 8,2015 na Juni 3,2016 washtakiwa hao wakiwa watumishi wa umma na waajiriwa wa TPDC kwa nafasi zao, wakati wakitimiza majukumu yao kwa makusudi walitumia madaraka vibaya.
Kwa kubadilisha na kupitisha bajeti na mpango wa mwaka wa manunuzi wa mwaka 2014/2015 na 2015/2016 kwa kuingiza ununuzi wa kifaa cha utafiti cha airborne gravity gradiometer survey ndani ya ziwa Tanganyika bila ya kupata kibali cha bodi ya wakurugenzi ya shirika.
Amedai kitendo hicho kinakiuka kifungu cha 49(2) cha sheria ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 kwa lengo la kujipatia manufaa yasiyohalali ya dola 3,238,986.50 ambacho ni sawa na Sh bilioni 7.2 kwa Bell Geospace.
Baada ya kusomewa shtaka hilo,washtakiwa wote walikana na upande wa mashtaka amedai upelelezi haujakamilika.
Hakimu Mashauri alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini bondi ya Sh 1 bilioni.
Wadhamini hao wametakiwa kuwa na barua za utambulisho kutoka viongozi wa mtaa, vijiji ama za waajili wao na vitambulisho.
Washtakiwa wasalimishe hati zao za kusafiria mahakamani na wasitoke nje ya jiji la dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama.
Kesi imeahirishwa hadi Machi 19,2018 kwa ajili ya kutajwa.Washtakiwa hao wanatetewa na wakili Deogratius Lyimo.
About Author Matukio360
Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.
No comments:
Post a Comment