Majaliwa awataka mabalozi kutangaza vivutio vilivyopo nchini...soma bari kamili na matukio360...#share

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchini Urusi na Rwanda kutumia fursa hiyo kwa kutangaza vivutio vilivyopo nchini ili kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii.
Pia amewataka Mabalozi kila mwisho wa mwaka wajifanyie tathmini ya mafanikio waliyoyapata kutokana na uwakilishi wao katika Mataifa ambayo  ni kwa kiasi gani wamechangia kwenye uboreshaji wa maendeleo ya Taifa.

Ametoa maagizo hayo jana (Jumapili, Aprili 8, 2018) wakati akizungumza na Balozi Ernest Mangu anayewakilisha Tanzania nchini Rwanda na Balozi Simon Mumwi anayewakilisha Tazania nchini Urusi, katika ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii ikiwa ni pamoja na uwepo wa mbunga za wanyama, hivyo ni vyema wanapoondoka wachukue nyaraka zote zitakazowasaidia katika kutangaza vivutio vya utalii ili kuongeza idadi ya watalii nchini.

Amesema mbali na kutangaza sekta ya utalii, pia watafute wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta nyingine kama vile madini, viwanda na kutafuta masoko ili wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi.

“Pia mkajifunze mbinu ambazo wenzetu wanazitumia katika kuboresha sekta mbalimbali ambazo na sisi tunazo hapa nchini kama za viwanda na kisha mje mtueleze namna ya kuziboresha. Kujifunza ni jambo zuri hivyo msisite kufanya hivyo huko muendako.”

Pia Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao wakawatambue na kuwaunganisha Watanzania waishio kwenye nchi wanazoiwakilisha ili nao washiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda na wawasisitize wafuate sheria za nchi wanazoishi na wakumbuke nyumbani.

Waziri Mkuu amewasisitiza mabalozi hao kwenda kupunguza gharama za uendeshaji wa Balozi kwa kuzuia matumizi katika mambo yasiyo ya lazima. “Pia maslahi ya nchi lazima mkayasimamie huko muendako hasa katika masuala ya kiuchumi.

Kwa upande wao mabalozi hao  wamesema watahakikisha wanayafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi wanazoziwakilisha.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search