Mhagama amwagiza Msajili vyama vya siasa kuchukua hatua kwa vyama vinavyokiuka sheria, miongozo...soma habari kamili na matukio360..#share

Na Mwandishi Wetu,
Dodoma
WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu
wenye Ulemavu Jenista Mhagama amemuagiza Msajili wa vyama vya Siasa
kuchukua hatua kwa vyama vinavyokiuka sheria na miongozo ya vyama vya siasa.
Ametoa kauli hiyo leo (Aprili 23,
2018) alipokuwa akitoa maelezo ya ufafanuzi juu ya hoja za ofisi yake,
zilizoainishwa katika Ripoti ya Mthibiti na Ukaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
kwa Mwaka wa fedha unoishia Juni 30, 2018 alipokutana na waandishi wa habari
Bungeni Dodoma.
Waziri Mhagama ameelekeza
kuhakikisha vyama vyenye mapungufu upande wa hesabu zao basi wawasilishe kwa
Msajili wa vyama ndani ya wiki 3 hadi 4.
“Namtaka Msajili wa Vyama achukue
hatua za Kisheria pasi kusita kwa chama chochote kinachokiuka sheria ya vyama
vya siasa Na. 2 ya mwaka 1992”.alisema Waziri Mhagama.
Aidha amemtaka Msajili wa Vyama
vya siasa nchini kuhakikisha anaweka miongozo na mpango kazi ili vyama
vilivyozoea kutowasilisha hesabu zao viache mara moja kwa mujibu wa sheria.
Waziri Mhagama aliongezea kuwa
taarifa ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilibaini mapungufu
kadhaa katika uendeshaji wa vyama vya siasa ikiwemo; Upungufu katika hesabu
zilizowasilishwa chini ya viwango vya Kimataifa vya uandaaji wa hesabu katika
sekta za umma na baadhi ya vyama kushindwa kuwasilisha hesabu zao kwa CAG kwa
ukaguzi
Pamoja na hayo alibainisha kuwepo
kwa vyama vya kisiasa visivyotumia rejista ya mali za kudumu ambapo vyama vinne
ikiwemo;CHADEMA, NLD,ADC na Demokrasia Makini havina Daftari la kudumu la mali
zao ikiwa ni kinyume na sheria zilizopo.
“Msajili wa Vyama nakuagiza kutoa
maelekezo kwa kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu kuwa na regista ya
mali zake ndani ya wiki tatu kuanzia leo kwani kukosa daftari la mali za kudumu
ni kinyume na kifungu Na.14(1)(b)(ii) ya sheria ya vyama vya siasa Na.5 ya
mwaka 1992.”alisisitiza Waziri.
Sambamba na hilo Waziri alimtaka
Msajili wa Vyama vya siasa kuhakikisha vyama vyote vinafuata miongozo
yote ya kihasibu ili kuondokana na mapungufu ya kukosekana kwa nyaraka za
malipo kama ilivyobainishwa na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ambapo
alibaini vyama vitatu kati ya tisa vina nyaraka pungufu ikiwemo CHADEMA, SAU na
ADC.
“Msajili wa vyama ahakikishe
vyama vya siasa vinatekeleza miongozo yote kihasibu pamoja na kanuni za fedha,
ambazo zinaelekeza nyaraka ziwe na viambatisho sahihi kwani ripoti ilibainisha
vyama vitatu vilikuwa na malipo yenye nyaraka pungufu zenye thamani ya shilingi
735,978,559 ambapo ni kinyume na miongozo ya kihasibu na kukosa uhalali wa
malipo hayo.”alisisitiza Waziri Mhagama.
Awali kifungu cha 14(1)(a) na
(b)(i) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 [RE: 2015] kinaelekeza kuwa,
kila chama cha siasa kinapaswa kutunza taarifa za mapato na matumizi, ikiwamo
taarifa za mali zake. Vile vile, kinapaswa kuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya
Siasa, taarifa ya hesabu zake zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG), pamoja taarifa ya mali zake.
Hivyo, Kifungu hicho kinampa
mamlaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi wa
hesabu za kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu. Katika mwaka wa fedha
unaoishia tarehe 30 Juni, 2017, CAG amefanya ukaguzi wa hesabu za Vyama vya
Siasa kumi ikiwemo; CCM, CHADEMA, NLD, TLP, Demokrasia Makini (MAKINI), TLP,
DP, SAU, AFP, CCK na ADC kati ya vyama vya siasa kumi na tisa vyenye usajili wa
kudumu. Vyama vya Siasa tisa (9) havikuwasilisha hesabu zake kwake kwa wakati
kwa ajili ya ukaguzi, hivyo hakukaguliwa.
No comments:
Post a Comment