Miguna Miguna asafirishwa kutoka Dubai kwenda Canada...soma habari kamili na matukio360...#share


Na Mashirika ya Kimataifa
MWANASIASA wa upinzani aliyezuiwa kuingia Kenya wiki iliyopita na kusafirishwa kwa lazima hadi Dubai ameelekea nchini Canada, vyombo vya habari nchini Kenya vimeripoti.
Miguna Miguna
Bw Miguna Miguna, ambaye ni wakili, amesafiri kwa ndege iliyokuwa ikielekea Toronto, Canada, baada ya kukaa katika uwanja wa kimataifa wa Dubai kwa siku nne.
Gazeti la Nation, limesema afisa mmoja wa serikali amewafahamisha kwamba Bw Miguna aliondoka Dubai akitumia ndege ya Air Canada 57 (ACA57) baada ya kuwasilisha pasipoti yake ya Canada.
Wakili huyo alikuwa amesema hakuwa na pasipoti hiyo alipowasili uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, Nairobi Jumatatu wiki iliyopita.
Wakili wake Cliff Ombeta hata hivyo ameambia BBC kwamba mteja wake hakuwa na pasipoti hiyo.
Aidha, amesema kwa sasa hawezi kuthibitisha iwapo Bw Miguna yumo safarini kuelekea Canada.
Safari ya ndege kutoka Dubai kwenda Toronto huchukua takriban saa 13.
Bw Miguna ndiye aliyeidhinisha kiapo cha Bw Raila Odinga alipokuwa anajiapisha kuwa 'Rais wa Wananchi' mwezi Januari.
Bw Miguna Miguna alijaribu kurejea Kenya Jumatatu lakini akazuiwa kuingia baada yake kudaiwa kutowasilisha pasipoti ya Canada ambayo ilitumiwa kumsafirisha kwa nguvu hadi Canada.
Wakili huyo alisisitiza kwamba ni raia wa Kenya na hafai kuzuiwa kurejea.
Taarifa zinasema Bw Miguna, ambaye pasipoti yake ya Kenya ilitwaliwa na polisi kabla ya kuondolewa kwake Kenya mwezi jana, alikuwa ametakiwa kuwasilisha ombi la kupata visa ya kukaa Kenya kwa miezi sita kwa kutumia pasipoti hiyo yake ya Canada.
Alikataa jaribio hilo na badala yake kutoa kitambulisho chake cha taifa kuonesha kwamba yeye ni Mkenya na kutaka aruhusiwe kuingia.
Bw Miguna, aliyekuwa amewasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mwendo wa saa nane adhuhuri, alikesha kwenye uwanja huo.
Maafisa walijaribu kumsafirisha kutoka uwanja huo mara ya kwanza kwa kutumia ndege ya shirika la Emirates ambayo ilikuwa inaelekea Canada kupitia Dubai usiku huo wa Jumatatu lakini hawakufanikiwa.


Hata hivyo, walifanikiwa usiku wa kuamkia Jumatano.

Bw Miguna asubuhi aliandika kwenye Facebook kwamba aliamka na kujipata yuko Dubai na kwamba anahitaji matibabu.
Mwanasiasa huyo alisema alisindikizwa na afisa wa idara ya ujasusi na kwamba amemuona daktari uwanja wa ndege.
Bw Miguna alisisitiza kwamba hatasafiri kwenda popote ila kurejea Nairobi.
Serikali imechukua hatua hiyo licha ya kuwepo kwa maagizo ya mahakama ya kuzuia kutimuliwa kwake na ya kuitaka serikali kufanikisha kurejea kwake nchini humo.
Jaji wa Mahakama Kuu George Odunga aliwapata na hatia waziri wa usalama nchini humo, mkuu wa polisi na mkuu wa idara ya uhamiaji ya kukaidi maagizo ya mahakama iwapo wangekataa kumwachilia huru.
Aliwatoza faini ya Sh200,000 (Dola 2,000) kila mmoja.


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search