Muhimbili kupandikiza figo wagonjwa 200...soma habari kamili na matukio360...#share

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili  (MNH) imeweka mipango ya muda mrefu na muda mfupi ili kuhakikisha huduma ya upandikizaji figo inakuwa endelevu, na imedhamiria kupandikiza figo kwa wagonjwa zaidi 200 kwa mwaka.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dare es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa MNH, Aminiel Aligaesha wakati akizungumza na waandishi wa habari  mara baada ya kuruhusiwa wagonjwa wawili ambao wamepandikizwa figo Aprili mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Amesema katika  mpango wa muda mfupi, kila mwezi hospitali hiyo itapandikiza figo wagonjwa watano, hivyo kwa mwaka itakuwa imefanikiwa kupandikiza figo wagonjwa 60.

“Mipango ya muda mrefu ni kuwa na sehemu maalum ya upandikizaji figo na hivi karibuni MNH itaanza ujenzi wa jengo jipya la ghorofa saba na katika jengo hilo tutatenga sehemu maalum ya upandikizaji figo , kila siku mgonjwa mmoja atapandikizwa figo, kwa wiki tutakuwa tumepandikiza figo wagonjwa watano, kwa mwezi wagonjwa 20 na kwa mwaka tutafanikiwa kupandikiza figo wagonjwa 240,’’ amesema Aminiel.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Magonjwa ya Figo  Muhimbili , Dkt. Jacqueline Shoo amesema tukio hilo ni la kihisoria kwani mwaka jana  hospitali ilifanikiwa kupandikiza figo mgonjwa mmoja  na Aprili mwaka huu hospitali hiyo imepandikiza figo wagonjwa wanne kwa mfululizo.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo MNH, Dkt. Onesmo Kisanga amesema takribani wagonjwa 800 nchini wanasubiri huduma ya upandikizaji figo na kati ya hao 50 tayari wameandaliwa.

Kwa upande wao wagonjwa waliopandikizwa figo na kuruhusiwa leo, Bi. Suzana John na Bi. Asha Athuman Kisebengo wameishukuru Hospitali ya Taifa Muhimbii  pamoja na waaalam wake kwa kuwapatia matibabu ya ubingwa wa juu ambayo awali hayakuwepo nchini.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search