Bei ya petroli, dizeli yashuka...soma habari kamili na matukio360...#share

Na Mwandishi Wetu,

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), juzi  ilitangaza kushuka kwa bei ya petroli na dizeli kwa asilimia 2.7 na asilimia 3.8; na ongezeko la asilimia 0.09 kwa mafuta ya taa.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Nzingagwa Mchany ilisema bei hizo mpya zitatumika Tanzania Bara kuanzia leo.

Hata hivyo, kwa watumiaji wa mafuta yanayopitia katika Bandari ya Dar es Salaam ni neema, lakini wa Bandari ya Tanga bei imeongezeka.

Mchany alisema mabadiliko hayo ya yanatokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na marekebisho ya bei yaliyofanywa na Ewura kutokana na kubadilika kwa tozo za wakala na Serikali za mitaa katika bidhaa hizo.

Ikilinganishwa na tangazo la bei ya mafuta la Aprili 4 kwa mafuta yanayopitia katika Bandari ya Dar es Salaam, bei ya petroli imepungua kwa Sh88 kwa lita (asilimia 3.8) na dizeli Sh61 kwa lita (asilimia 2.75); huku bei ya mafuta ya taa ikiongezeka kwa Sh2 kwa lita sawa na asilimia 0.09.

Tofauti na wanunuzi wa rejareja, bei ya wale wa jumla upande wa petroli imepungua kwa Sh100.91 kwa lita (asilimia 4.58), dizeli Sh73.71 kwa lita (asilimia 3.52) na mafuta ya taa Sh10.49 kwa lita sawa na asilimia 0.51.

Mafuta yanayopita Bandari ya Tanga bei kwa wanunuzi wa rejareja imeongezeka kwa asilimia 0.14 kwa petroli na asilimia 0.71 kwa dizeli.

Lakini wauzaji wa jumla bei imepungua kwa asilimia 0.46 (Sh9.8 kwa lita) kwa petroli na asilimia 0.1 (Sh1.9 kwa lita) kwa dizeli.

“Hakuna uingizaji mpya wa mafuta uliofanyika nchini kupitia Bandari ya Tanga, lakini kutokana na mabadiliko ya bei ya Ewura kuna mabadiliko ya bidhaa hizo tofauti na ilivyotangazwa Aprili 4,” alisema Mchany na kuongeza:

“Bei ya petroli itaongezeka kwa Sh3 kwa lita, huku dizeli ikiongezeka kwa Sh15 kwa lita.”

Kutokana na kupungua kwa mafuta ya taa katika Bandari ya Tanga, Ewura imewashauri watumiaji wa mikoa ya Nyanda za Juu kuchukua bidhaa hiyo katika Bandari ya Dar es Salaam kwa bei elekezi.

Taarifa ya Mchany inasisitiza kila kituo cha kuuzia mafuta kuchapisha bei kwenye mabango yanayoonekana bayana na kituo kutoa risiti za kielektroniki (EFD) kwa kila mauzo.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search