Dk. Ndugulile: Hakuna mtu aliyethibitika kuwa na ugonjwa wa Ebola...Soma habari kamili na matukio360...#share

NA WAMJW-DAR ES SALAAM.

NAIBU Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto Dk. Faustine Ndugulile amethibitisha kuwa hakuna mtu aliyethibitika kuwa na ugonjwa wa EBOLA hapa nchini wala hakuna ugonjwa huo hapa Tanzania.

Hayo ameyasema leo jijini Dar es salaam mbele ya waandishi wa habari wakati akitoa tamko kuhusu ugonjwa wa EBOLA kama ilivyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwepo kwa ugonjwa huo hapa nchini.

“Napenda kuwatoa hofu watanzania kwamba hakuna ugonjwa wa EBOLA na wala hakuna mtu aliyethibitika kuwa na ugonjwa huo, hivyo tuendelee na shughuli za kujenga Taifa ila tunatakiwa tuchukue tahadhari za kujikinga juu ya ugonjwa huu” alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha, Dkt. Ndugulile amesema kuwa katika kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa EBOLA usiingie nchini Serikali imeweka vifaa vya kupima joto la mwili (themo scaner) pia wapo wataalamu wa Afya ambao  wanauliza hali ya wageni wanaoingia katika mipaka yote inayoizunguka nchi yetu ili kuzuia ugonjwa huo kuingia.

Dkt. Ndugulile amesisitiza kuwa, Serikali haijafunga mipaka ya nchi kwa sababu ya kujikinga na EBOLA.

“Tanzania hatujafunga mipaka na hatuwezi kufunga biashara za mipakani ila tumeimarisha ufuatiliaji wa watu wanaoingia nchini hususani maeneo ya viwanja vya ndege na mipaka mingine yote.”

Mbali na hayo Dkt. Ndugulile ameitaka mikoa yote iliyo mipakani kudhibiti watu wote wanaoingia nchini kwa njia za panya ili kuepusha uingizaji wa ugonjwa huo kwa wananchi  huku akiwataka wafanyabiashara wa mipakani kutoa ushirikiano ili kudhibiti ugonjwa huo usiingie nchini.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani ambaye pia ni Afisa wa kushughulikia magonjwa ya kuambukiza Dkt. Grace Saguti amesema kuwa Wananchi wanatakiwa kupata elimu juu ya kujikinga na ugonjwa huo.

“Elimu inahitajika ya kutosha kwa wananchi wote hasa katika kufichua wagonjwa wa Ebola kama watagundulika hasa wanaotoka nje ya nchi ili kupata msaada kutoka kwa watoa huduma za afya walio yao juu ya kujikinga na ugonjwa huo.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search