Serikali kuendelea kuhakikisha watanzania wanapewa fursa za ajira...soma habari kamili na matukio360...#share
WAZIRI Mkuu Kassim
Majaliwa amesema Seriali ipo makini na ajira za wageni na itaendelea
kuhakikisha kuwa Watanzania wanapewa fursa kwanza.
Ametoa kauli hiyo
leo asubuhi (Alhamisi, Mei 17, 2018) Bungeni mjini Dodoma katika kipindi
cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa
Viti Maalumu, Bi. Leah Komanya aliyetaka kupata kauli ya Serikali juu ya wageni
wanaoingia nchini na kupata ajira kwenye maeneo nyeti kama vile bandarini au
viwanja vya ndege.
“Ajira zote za
wageni nchini Tanzania ni kwa nafasi zile za kitaalam tu ambazo Watanzania
hawana uwezo nazo na hatujaacha wazi, tumeweka ukomo kuwa ni wageni watano tu
kwa kila taasisi ndio wanapata fursa ya kuajiriwa ndani ya nchi, kuitumikia
taasisi hiyo na ni kwa nafasi ambazo watanzania hawana uwezo nazo,”
amesisitiza.
Akifafanua zaidi,
Waziri Mkuu amesema pale ambapo italazimu raia wa nje apate ajira, Serikali
itaendelea kusimamia ili kuhakikisha kama kweli nafasi hiyo haina mtu na ni
nafasi nyeti yenye utaalam ambao hakuna Mtanzania mwenye uwezo nayo.
Akijibu hoja kuhusu
wageni kufanya kazi kwenye maeneo nyeti, Waziri Mkuu amesema Serikali
imeendelea kuhakikisha kwamba hakuna mgeni anayefanya kazi kwenye maeneo ya
viwanja vya ndege, bandari au yale ya mipakani. “Hii ni kwa sababu ni lazima
tuweke Watanzania ambao kweli wanakerwa na nchi yao na wanaweza kulinda nchi
yao kuanzia mipakani ili kuhakikisha kwamba hakuna jambo lolote linaloashiria
kuvunjika kwa amani.”
Amesema endapo
atakutwa mtu yeyote wa Taifa la nje anafanya kazi kwenye maeneo hayo, basi
atakuwa ameajiriwa na kampuni ambayo inafanya shughuli maalum kwenye eneo hilo
na kwa masharti yale yale kwamba watapata nafasi kufanya kazi kwenye kampuni
hiyo kama nafasi hiyo hakuna Mtanzania mwenye uwezo nayo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, MEI 17,
2018.
No comments:
Post a Comment