Manispaa ya Ilala yaokoa sh.bilioni 1.5 kwa kipindi cha Januari hadi Machi, 2018...soma habari kamili na matukio360..#share


Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam

HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam imeokoa sh.bilioni 1.5 kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi 2018 kutokana na kushinda kesi saba.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na  Kaimu Mwenyekiti wa kamati ya fedha na utawala, Waziri Mweneviale alipokuwa akisoma taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya kamati hiyo kwa robo mwaka ya kipindi hicho mbele ya Baraza la Madiwani na kujadiliwa.

Taarifa nyingine za Utekelezaji wa Majukumu zilizosomwa mbele ya Baraza hilo na kujadiliwa ni za kamati ya Fedha, Uchumi na Huduma za jamii pamoja na kamati ya Mipango Miji na Mazingira.

“Halmashauri imefanikiwa kushinda kesi takribani saba ikiwemo kesi Na. 54/2003 kati ya Charles Moses dhidi ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ambapo mdai alikuwa akiidai halmashauri kiasi cha Tsh 1,500,000,000 hivyo kwa kipindi hicho kamati imeokoa kiasi hicho cha fedha,” amesema Mweneviale.

Ameeleza kuwa kwa kipindi hicho kamati imefanikiwa kusimamia mapato na matumizi ya halmashauri ambapo imeweza kukusanya jumla ya sh.10,348,333,506 sawa na asilimia 88 ya makisio ya sh.11,793,447,388.50 bila kuweka kodi ya majengo ya sh 800,000,000.00 ambazo zinakusanywa na Serikali kuu .

Mwenenviale ameongeza kwamba kamati hiyo imeidhinisha matumizi ya force account kwa ajili ya ujenzi wa ukuta wa pavement katika hospitali ya Mama na Mtoto Chanika kwa gharama ya sh.183,864,091.20.

Amebainisha kuwa kamati hiyo imeweza kusimamia uchangiaji wa mapato ya ndani kwenye miradi ya Maendeleo kwa asilimia 60% na kwamba halmashauri ilichangia jumla ya shilling 3,900,000 kwenye Akaunti ya Maendeleo ikiwa ni sawa na asilimia 80% ya kiasi kilichopangwa kwa kipindi hicho cha January hadi Machi.

Kwa upande wa  taarifa ya kudumu ya kamati ya Uchumi na huduma za jamii iliyosomwa na Kaimu Mwenyekiti, Helen Lyatula, amesema kamati hiyo imefanikiwa kwa kipindi hicho kusimamia utekelezaji wa shughuli mbali mbali za miradi ya maendeleo.

Amesema moja ya miradi waliyosimamia ni taaluma na nidhamu katika shule zote za awali na msingi za serikali na zisizo za serikali, kutoa muongozo na taratibu mbalimbali za kufanikisha malengo waliyoweka kulingana na sera ya elimu na kuongeza kwamba inatarajiwa jumla ya walimu 1653 wa shule ya msingi watapandishwa vyeo na madaraja.

“Jumla ya walimu 1653 wa shule ya msingi wanatarajia kupandishwa vyeo na madaraja, lakini halmashauri pia imepokea vitabu 100, 904 toka TAMISEMI na kusambaza kwa shule zote msingi,” amesema Lyatula.

Aidha amesema pamoja na mafanikio waliyoyapata bado kumekuwepo na changamoto zinazokabili idara na vitengo katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa madai ya likizo hadi sasa jumla ya walimu wa shule za msingi 1837 wanadai kiasi cha sh 478,346,684,00, pamoja na ukomo wa bajeti katika utekelezaji shughuli mbalimbali za kilimo, ushirika na umwagiliaji.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Mipangomiji na Mazingira Greyson Siwilwa, akisoma taarifa ya kamati hiyo amesema kwa kipindi hicho imeweza kusimamia utekelezaji wa shughuli mbali za uendeshaji wa miradi ya maendeleo kupitia Idara ya Mipangomiji na Ardhi, Ujenzi, Maji na Uthabiti  wa Maji Taka na Uhifadhi wa Mazingira na Udhibiti wa taka ngumu.
 


 

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search