SERIKALI YATANGAZA AJIRA MPYA 52,436
![]() |
| Waziri Angela Kairuki |
Serikali inakusudia kuajiri watumishi wapya 52,436 katika
mwaka ujao wa fedha. Ajira hizo ni tofauti na zile za madaktari 258 na
wataalamu wa Afya 11 waliotangazwa kuajiriwa Jumatano wiki hii baada ya
kupeleka maombi na kukidhi vigezo kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya kwenda kufanya kazi nchini kenya.
Akizungumza Bungeni jizi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, wakati
alipofanya majumuisho yake kwa mwaka ujao wa fedha wa 2017/2018 alisema:
“Tunatambua umuhimu wa rasilimali watu wanaotosheleza kama
nilivyoeleza wakati nasoma bajeti kuwa tulishatoa vibali 9,700 vya ajira na
tayari wameshaingia kazini.”
“Namshukuru Rais kwa kuona umuhimu wa kuajiri madaktari 258
na kwamba Jumatatu wanaanza kazi rasmi” alisema.
Alisema wataenelea kuajiri kwa awamu na watahakikisha kwamba
hawarudii makosa yaliyotokea ikiwamo watumishi hewa.
Pia alisema zaidi ya maofisa 1,595 waliosababisha kuwapo kwa
watumishi hewa 19,708 wamechukuliwa hatua na kwamba wengine wana kesi
mahakamani.
Alisema watumishi hao hewa walibainika wakati wa uhakiki
katika orodha ya malipo ya mishahara, hivyo waliondolewa na kama wangeachwa
wangeigharimu serikali TZS bilioni 19.8 kwa mwezi.
“Kumekuwa na malalamiko kuwa serikali hii ni ya kuhakiki tu.
Naomba niwaeleze kuwa hatuwezi kukaa na watumishi bila kujua kila mmoja ana
sifa zipi na weledi au anatekeleza wajibu wake kwa kiasi gani.”
“Tutaendelea na mpango huu wa uhakiki na kwamba ni endelevu
na tutaendelea kufanya hivyo wala hatutishiwi na maneno ya watu”
“Kupitia uhakiki tuliofanya watumishi zaidi ya 19,708
wamebainika katika orodha ya malipo yetu ya mishahara na waliondolewa,
tungewaacha wangeigharimu serikali kwa mwezi shilingi bilioni 19.8”
“Maofisa zaidi ya 1,595 wa madaraka mbalimbali walioshiriki
kuwepo kwa watumishi hao hewa tumewachukulia hatua na kwamba wengine wana kesi
mahakamani na tayari shilingi bilioni 9.3 zimesharudishwa hazina” alisema.
Angellah alisema Serikali ilifanya uamuzi wa uhakiki kwa nia
njema na itetenga fedha ili kukamilisha mchakato wa utambuzi na uandikishaji.
Aliwataka waajiri wote nchini kuweka kipaumbele katika
kuandaa umuhimu wa mafunzo kwa watumishi wao.
Alisema kwa mwaka wa fedha 2015/2016 watumishi 395
walipatiwa mafunzo nje ya nchi na katika mwaka wa fedha 2017/2018 watumishi wa
umma 654 nao walipatiwa mafunzo.
“Tunayo sera ya mafunzo ambayo inasisitiza waajiri kuweka
vipaumbele katika kuandaa umuhimu wa mafunzo kwa watumishi wao ambayo
itazingatia mahitaji yao halisi. Kupitia ofisi yangu idara ya rasilimali watu
wamekuwa wakitafuta fursa ya mafunzo nje ya nchi ili kuhakikisha watumishi
wengi wanaweza kujiendeleza.”
“Natoa rai kwa waajiri kama ambavyo wanatenga fedha kwa
kuzingatia masuala mbalimbali, ni vyema katika bajeti zao wayape kipaumbele
mafunzo kwa watumishi wao. Tusitafute visingizio eti kwa sababu hakuna fedha”
alisema.
Kwa upande wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (Tamisemi) George Simbachawene, alisema kwa mwaka ujao wa
fedha wa 2017/208, serikali imetenga bilioni 96.3 kwa ajili ya kununua dawa.
Alisema kumekuwa na upungufu wa watumishi 96,000 huku
waliopo wakiwa ni 46,000.
Kuhusu madeni ya walimu, alisema madeni yote ambayo si ya
mshahara wameshayalipa.
Akijibu hoja za wabunge kuhusu kuwapo migongano ya uongozi
inayosababishwa na wakuu wa mikoa na wilaya alisema:
“Kwanza hao wanaotajwa wapo kwa mujibu wa sheria hivyo
hakuna namna lazima waelewane”
source: swahilitimes




No comments:
Post a Comment