WASIFU MATUKIO: MFAHAMU MSOMI PROF. KITILA MKUMBO - KATIBU MKUU WIZARA YA MAJI NA UMWAGILIAJI...
![]() |
| Prof. Kitila Mkumbo akila kiapo mbele ya Rais John Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam |
Prof. Kitila Mkumbo Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji; Mhadhiri Msomi wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na mwanaharakati wa masuala ya kisiasa. Alizaliwa tarehe 21 Juni 1971 katika Kijiji cha Mgela wilayani Iramba, Singida. Prof. Kitila hakuwa na bahati ya kulelewa na wazazi, hivyo alisomeshwa kwa misaada ya ndugu na wasamaria wema.
Alisoma katika Shule ya Msingi Mgela iliyoko wilaya ya Iramba kati ya mwaka 1981-1987 kisha akajiunga Shule ya Sekondari Mwenge (Singida) na kusoma kidato cha kwanza hadi cha tano mwaka 1988-1991 na elimu ya Juu ya Sekondari akaipata pale Shule ya Sekondari Pugu kati ya mwaka 1992-1994 akijikita katika mchepuo wa PCB (Fizikia, Kemia na Bailojia).
Baada ya kuhitimu kidato cha sita alifanya kazi ya kuvua samaki katika Bwawa la Mtera huko Iringa kwa sababu ya kuwa na hali mbaya ya kiuchumi na baadaye alipata nafasi ya kwenda kujiunga na mafunzo ya polisi kwenye Chuo cha jeshi CCP Moshi kwa muda wa miezi miwili lakini alikatisha mafunzo baada ya kuchaguliwa kujiunga Chuo Kikuu.
Prof. Kitila alihitimu shahada yake ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam mwaka 1999 akisomea Sayansi ya Elimu akaanza kazi hapo hapo Chuo Kikuu kama Ofisa Utawala, aliifanya kazi hiyo kwa miaka minne (1999 – 2003) na wakati anafanya kazi aliendelea kusoma shahada ya uzamili/umahiri (M.A) akibobea katika Saikolojia, alihitimu shahada hiyo mwaka 2002.
Kitila alifanya vizuri katika shahada ya umahiri na baada ya kufundisha Chuo Kikuu kwa miaka michache alipewa udahili katika Chuo Kikuu cha Southampton kilichoko nchini Uingereza ambako alitunukiwa shahada ya uzamivu akibobea pia katika saikolojia, hii ilikuwa ni mwaka 2008.
Kati ya mwaka 2009 – 2012, Prof. Kitila amefanya kazi kama mratibu wa kamati ndogo ya ufundi ya masuala ya UKIMWI lakini pia kuanzia mwaka 2010 hadi hivi sasa ameendelea kuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TCIB (Tanzania Citizens Information Bureau (TCIB).
Mwaka 2010 hadi 2012 amekuwa Makamu Mwenyekiti wa UDASA (Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam) na kisha akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UDASA Oktoba 2014 na anaendelea na wadhifa huo.
Mwaka 2009 alikuwa Ofisa anayesimamia mitihani katika Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, amekuwa mhariri mkuu na mhariri msaidizi wa machapisho mbalimbali yanayohusu elimu ya saikolojia, sanaa na sayansi.
Pia, amekuwa mkuu wa Idara ya Elimu ya Saikolojia na masomo ya Mtaala katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaama kuanzia mwaka 2009 – 2012, amekuwa Mhadhiri Mwandamizi kuanzia mwaka 2011 – 2014, amekuwa Mkuu wa Kitivo cha Elimu katika Chuo Cha Elimu cha Dar Es Salaam (DUCE) na kufanikiwa kuwa Profesa Mshiriki katika Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kuanzia Julai 2014.
Kitila alianza siasa kama mwanachama wa CCM, baadaye alijiunga CHADEMA kawa mshauri muhimu wa chama hicho. Naweza kuthubutu kusema, kati ya wasomi na wataalam waliotoa mchango mkubwa kiushauri, kiuhaulishaji na kimkakati na kuifanya CHADEMA iwe chama kinachojiendesha kisasa sana leo hii, mmoja wa wasomi hao ni Prof. Kitila.
Mwaka jana (2014), Prof. Kitila alifukuzwa katika chama chake cha zamani (CHADEMA) kwa tuhuma za kuandaa waraka wa mapinduzi na kukihujumu chama hicho, Kitila alitangaza kuwa angeshirikiana na wenzake kuanzisha chama kipya ambacho hivi sasa kinajukana kama ACT – Wazalendo. Na hata rafiki yake wa siku nyingi, Zitto Kabwe amekweishjiunga na chama hicho. Hata katika chama hiki kipya yeye amekuwa mshauri mkuu. Watu nilioongea nao kutoka ndani ya ACT wanasisitiza kuwa Kitila ana mchango mkubwa na unaoonekana anapokuwa katika taasisi yoyote ile.
Prof. Kitila amekwishafanya tafiti zaidi ya 18 na zimechapishwa katika majarida ya kitaaluma ya kimataifa, amekwishaandika vitabu takribani vitatu, ameoa na ana watoto watatu.
MBIO ZA UBUNGE
Prof. Kitila hakuwahi kugombea ubunge katika jimbo lolote hapa Tanzania, muda wake mwingi amejikita katika masuala ya kitaaluma na ushauri wa mikakati ya kisiasa. Japokuwa alipokuwa mwanachama hai wa CHADEMA alifanya harakati nyingi katika jimbo la Iramba, (jimbo linaloongozwa na Mwigulu Nchemba wa CCM) na amewahi kuingia kwenye misukosuko mingi na hata kufunguliwa kesi ya kisiasa kwa sababu ya harakati zake.
NGUVU YAKE
Sifa na nguvu ya kwanza ya Prof. Kitila ni kuwa kijana na msomi mahiri. Pamoja na kuwa wasomi wengi wanapewa madaraka na wanavurunda kama vile hawakwenda shule, bado mataifa yote duniani hayakwepi wala kukimbia dhana ya kuongozwa na watu walioelimika maana kuna wasomi wengi tu ambao ni waadilifu sana katika kazi zao, mmoja wao ni Prof. Kitila. Ukiniuliza mmoja kati ya wasomi wanaojua majukumu yao na wanayasimamia sana, ntakwambia Prof. Kitila ni mmoja wao. Nguvu na sifa hii vina maana kubwa sana kwa mtu ambaye anafikiri au anafikiriwa kuwa rais wa nchi.
Lakini jambo la pili, yeye ni mwanademokrasia thabiti na anayependa demokrasia iwe katika vitendo. Msomi huyu ni mmoja wa watu wanaoamini katika kujenga hoja na wanaopenda hoja zishindanishwe na zijadiliwe kwa uwazi na kisha hoja yenye mashiko ndiyo ipitishwe na kukubaliwa na pande zote kwa sababu ina tija kwa jamii au taifa.
Ukitembelea ukurasa wake wa “Facebook” utaona watu wanaandika jambo lolote na humuoni akigombana nao, anapingwa waziwazi na wakati mwingine anatukanwa lakini anaacha uhuru wa wanaompinga na kumtukana uendelee. (Mimi binafsi nimekuwa sipendi mtu anitukane au anidhalilishe kwenye mitandao, napenda kupingwa kwa hoja na si kutukanwa, na nakumbuka kila aliyenitukana niliishia kumuondoa miongoni mwa marafiki).
Prof. Kitila yeye ameenda mbali zaidi, yuko tayari kwa hoja na yuko tayari hata kutukanwa na kudhalilishwa, mwisho wa siku kila mtu huendelea kuwa rafiki yake kwa muktadha huo. Sifa hii ni ngumu mno kuipata kwa wanasiasa wengi, uvumilivu wao una ukomo lakini kwa Kitila ni tofauti. Nchi kama yetu inahitaji watu wa namna hii kwenye uongozi wa juu.
Itaendelea kesho..........
Source: Mchambuzi Mashuhuri Julius Mtatiro




No comments:
Post a Comment