Kitaifa: Wenye vyeti feki waachwa njia panda, Serikali yasema hatima yao ni baada ya mchakato wa uhakiki wao kukamilika...#share
WAZIRI
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki amesema Serikali haijatoa
tamko kuhusu hatma ya mafao ya watumishi wa umma waliokutwa na vyeti feki huku
akibainisha tamko litatolewa baada mchakato wa uhakiki vyeti hivyo kukamilika.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dar
es Salaam wakati akizungumza na Watumishi wa Manispaa ya Kinondoni, amesema kumekuwepo
na taarifa za upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kwa namna tofauti
tofauti jambo hilo, hali inayosababisha sintofahamu miongoni mwa wahusika na
kusisitiza ufafanuzi utatolewa uhakiki utakapokamilika.
"Hakuna sehemu tuliyosema
watalipwa au hawatalipwa mafao yao ifikapo mwisho wa uhakiki Serikali itatoa
ufafanuzi," alisema Kairuki.
Waziri Kairuki amewataka
watumishi wa manispaa nchini kuacha tabia ya kusambaza taarifa za Serikali
kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka
2015.
Ameongeza kuwa changamoto
zinazoikabili manispaa ya Kinondoni zitatafutiwa ufumbuzi zikiwemo za upungufu
wa walimu 50 wa shule ya msingi,
watumishi 371 wa afya pamoja na watumishi wa ardhi na mipango.
Amewakumbisha maafisa utumishi wa
manispaa hiyo kuwafanyia uhakiki watumishi kabla yakuwaingiza katika mfumo
malipo ya mishahara na kwamba Serikali kwenye bajeti ya mwaka 2017/18 kuanzia mwezi huu hadi wa tisa itatoa vibali
52,476 vya ajira mpya.
Amewashauri watumishi hao
kujikinga na Ukimwi kwa kubadili mienendo yao pamoja na kushiriki kufanya
mazoezi ili kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza.
Kwa upande wake Afisa Utumishi
Mkuu wa manispaa hiyo, Anna Mwakalyelye alisema hadi sasa mashauri ya nidhamu
134 yanashughulikiwa, 48 yameshashughulikiwa huku 80 yakiendelea kufanyiwa
kazi.
Amesema manispaa tayari
imeshatenga fedha za kujenga na kuzifanyia ukarabati Ofisi za kata
zinazopatikana katka manispaa ya Kinondoni.
Amefafanua kuwa watumishi 372
walipandishwa vyeo na tisa kufanyiwa mabadiliko ya vyeo kulingana na vigezo
walivyonavyo.
Pia amesema watumishi wanaendelea
kupatiwa mafunzo ambayo lengo ni kuwasaidia kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,
Ali Hapi alimpongeza waziri Kairuki kwa utendaji kazi wake na kumuomba atizame
kero zinazoikabili ikiwemo upungufu wa watumishi idara ardhi na mipango ambapo
wanaofanya kazi wapo wanane wanaohudumia takribani watu milioni 1.3.
Na Hussein Ndubikile
No comments:
Post a Comment