Morning Talk: Lissu 'apasuka'.. "Sipendi, lakini Siogopi, Ndio Maana Siachii.." ataka wafadhili wasitupe 'Fedha'.. Balozi Mahiga akanusha Tanzania 'kuichokonoa' Kenya.. #SHARE.. na tamko la CUF kuinusuru CHADEMA na kamata-kamata..


Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema hapendi kukamatwa na vyombo vya dola kwa kuwa mahabusu si mahala pazuri pa kuishi watu hususan wasiokuwa na hatia, hata hivyo amesema kitendo hicho hakitamuogofya na kuzuia harakati zake za kupaza sauti.
Lissu ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wanahabari kuhusu matukio ya baadhi ya viongozi na wafuasi wa Chadema kukamatwa na vyombo vya dola, na kuwekwa mahabusu.
“Sipendi kukamatwa mahabusu si pazuri, lakini inafikia hatua inabidi uamue kama kwenda machinjoni ukiwa umenyamaza kimya au kuingia huku unapiga kelele mataifa yasikie,” amesema.
Lissu ambaye mpaka sasa ana kesi za jinai takribani nne katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ikiwemo ya uchochezi, amedai kuwa baadhi ya viongozi na watumishi wa umma wako katika hali ya hofu katika utendaji kazi wao, huku akiwataka wananchi kupaza sauti ili hali hiyo iondolewe.
“Hofu kila mahali, mahakamani na hata kwenye utumishi wa umma hakuna aliyeko salama. Viongozi wa dini wako kimya wandhani wako salama. Tunahitaji kupaza sauti kila mmoja kwa nafasi yake,” amesema.
Na Regina Mkonde - Mo blog



==================================
Timu ya Kagera Sugar ya Bukoba imeanza mazoezi yake ya kujianda katika msimu mpya 2017/2018 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza Agosti 26, mwaka huu katika uwanja wa Karume ikiwa ni kambi yake ya awali kufanyika Jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na wanahabari mratibu wa timu hiyo Mohamed Hussen amesema lengo la kuweka kambi Jijini Dar es Salaam nikuweza kupata mechi nyingi za kirafiki ili waweze kujijenga zaidi.

"Tumeanza mazoezi leo hapa Dar, tutakuwa hapa kwa majuma mawili na baada ya hapo tutarejea kwenye kambi yetu ya kudumu mkoani Kagera lengo la kuanzia kambi hapa Dar es Salaam nikupata michezo mingi ya kirafiki kabla ya kuanza kwa ligi kuu ambapo tutanzia nyumbani Kaitaba dhidi ya mbao ya Mwanza ", amesema Hussen.

Pamoja na hayo, timu ya Kagera Sugar imetua Jijini Dar es Salaam ikiwa na wachezaji wote wapya sita, wakiongozwa na beki maarufu wa zamani wa Simba, Juma Said Nyosso, ambaye amerejea kwenye soka baada ya kumaliza adhabu ya kufungiwa miaka miwili baada ya kufanya kitendo cha utovu wa nidhamu uwanjani ambapo kwa sasa ndiye mchezaji aliyeweza kuweka rekodi ya kufungiwa muda mrefu kujihusisha na soka nchini Tanzania.

Kwa upande mwingine, wachezaji wengine waliosajiliwa Kagera Sugar ni pamoja na Said Kipao, Peter Mwalyanzi, Omary Daga ‘Dagashenko’, Venance Ludovic pamoja na Japhary Kibaya. - EATV

===========================
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema kinalaani, kitendo kilichoanzishwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kuwakamata viongozi wa vyama vya upinzani na kuwaweka rumande pasipo makosa yoyote.



Kauli hiyo ya CUF imetolewa jana na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano, Salim Bimani ambapo takwimu zinaonesha katika kipindi cha mwezi mmoja zaidi ya viongozi 70 wa vyama upinzani hasa Chadema wamekuwa wakikamatwa na polisi kwa maagizo ya wakuu wa wilaya na mikoa kwa kutumia mamlaka waliyonayo kisheria ya kumuweka mtu rumande kwa masaa 48.

Alisema kadhia iliyotokea hivi karibuni mkoani Ruvuma ya kumkamata na kumuweka ndani Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Vincent Mashinji pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ndanda ambae pia ni Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini Cecil Mwambe, Mbunge Viti Maalum Kanda ya Kusini Zubeda Sakuru na viongozi wengine ni ukiukwaji, haki za binadamu na utawala bora.

Alisema vitendo hivyo vya kamatakamata ni muendelezo wa utekelezaji wa maagizo kutoka juu katika kudhibiti harakati za vyama vya upinzani, ambapo ni kinyume na Sheria za Vyama vya Siasa na Katiba ya nchi ibara 20 (1).

“Ibara hiyo inasema kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo,” alisema.

Vilevile alisema Ibara 21 (2) inasema kila mtu anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kifikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu yeye, maisha yake au yanayolihusu Taifa.
Bimani alisema CUF inasikitishwa kukamatwa kwa katibu mkuu wa Chadema akiwa katika kikao cha ndani akikagua shughuli za chama katika majimbo ya kanda.

Mkurugenzi huyo alisema hoja za polisi kumtaka katibu huyo atoe maelezo kwa nini yumo katika mkoa huo na amekwenda kufanya nini ni hoja isiyo na mashiko kwa mtu wa hadhi yake.

“Hivi angekuwa ni katibu mkuu wa CCM angethubutu kumkamata na kumuuliza maswali kama hayo,” alihoji?

Alisema CUF inamuasa Mwenyekiti wa CCM, John Magufuli, asiyatumie vibaya madaraka yake ya Urais aliyopewa na wananchi katika kudhibiti upinzani kama sehemu ya maandalizi ya kukinusuru chama chake na chaguzi zijazo za 2019 na 2020.

Alisema wananchi wanapochoka huwa hawalazimishwi cha kufanya hivyo kumtaka acha wafanye maamuzi wenyewe, na kwamba kuwadhibiti wapinzani hakutokusaidia bali ni kuhatarisha amani ya nchi kwa kuwajenga mazingira ya chuki na hasira.


========================














About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search