GUMZ KISPOTI: Aug. 23 Leo Tuelekee Taifa 'kuwadeki' watani.. 'Onesheni viwango, mdhihirishe ukongwe wenu katika soka'.. #share
NI wakati mwafaka sasa. Ndiyo! NI wakati tuliokuwa tukiusubiri sana kuona vile viwango vilivyokuwa vikisemwa na viongozi na mashabiki kuhusu wachezaji waliokuwa wakiwasajili kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Usajili huu uliwavuta wengi. Familia ya soka inaamini kabisa kuwa, sasa utamu wa soka katika ligi yetu utaonekana.Wapo waliosema kuwa, mwaka huu lazima ubingwa waupeleke Tukuyu, samahani, waupeleke kwenye makao makuu ya klabu yao.
Hata ule utani wa soka, sasa umebaki jina. Ndiyo umebaki jina. Unakataa nini? Kama umesajili wachezaji nyota, tena kutoka mataifa yaliyopiga hatua katika soka. Tunaweza kusema ni kama vile soka la Burkina Fasso na Brazil.
Ni sheeda tena ni sheeda kweli.Wapo waliotamba na hata kusema kuwa, wanaweka kambi Brazil kwa ajili ya timu fulani. Wapo waliosema kuwa, ubingwa ni wetu. Kweli inapendeza.
Maisha ya soka hasa ukiwa familia ya soka wakati wa usajiri unanenepa kwa maneno ya viongozi wa klabu yako. Unasuuzika kwa maneno matamu na tambo zinazotolewa na viongozi wetu.
Kweli familia ya soka wakati wa usajili tunaonekana kama mbumbumbu. Ni kweli mbumbumbu. Hata wataalamu wa soka nao hutoa michengo yao kwa vyombo vya habari wanapoulizwa ubora wa wachezaji wanaosajiliwa.
Soka ni starehe. Soka ni amani, soka ni kiburudisho kizuri kwa watu wa mataifa mbalimbali. Soka linachangia kuleta amani sehemu palipo na machafuko. Ndiyo maana linapendwa sana na watu wengi duniani.
Oh! Upande wangu ninachoka sana. Ninachoka kwani katika kipindi chote cha maisha na uelewa wangu wa soka, hizi kelele zimekuwa kama utamaduni. Tena utamaduni wa klabu mbili kubwa kongwe. Sasa imeongezeka nyingine.
Ndiyo! Kwani uongo. Sauti ya Banyambala inapaa. Sauti ya Banyambala inagusa nyoyo za mashabiki na viongozi wetu wa soka. Viongozi wenye mawazo ya kutamba katika ligi ya nyumbani.
Hivi klabu za Tanzania zinafanya usajili kwa ajili ya ligi ya nyumbani? Hivi hawa viongozi wanasaka umaarufu hapa hapa nyumbani? Duh! hii n i kali tena kali kweli. Naweza kusema wana mawazo mgando.
Mh! Acheni nigune mimi. Inasikitisha sana. Sauti ya Banyambala tangu miaka ya nyuma, imekuwa ikipaza sauti, lakini viongozi wetu wa soka wameziba masikio yao. Hivi hata macho hayaoni?
Mechi moja ama mbili tu, utasikia kocha hana uwezo. Watamtafutia sababu hata kumfukuza kazi. NI uonevu mkubwa na udhalilishaji wa taaluma. Ndiyo ni udhalilishaji huo.
Hebu viongozi wa klabu wapeni makocha kazi ya kusajili. Wapeni uhuru huo waifanye kazi hiyo ya usajili. Wakisajili wachezaji wabovu, hapo mtakuwa na kauli ya kuwatimua. Lakini unampofanya usajili nyie, kisha mnawafukuza makocha, huo ni udhalilishaji wa taalumu ya ukocha.
Ukweli Sauti ya Banyambala inawataka kwanza, viongozi muwe wa kwanza kujiuzulu, kwani ninyi ndiyo mliosajili wachezaji wabovu na si makocha. Acheni kuchezea taaluma ya watu.
Sauti ya Banyambala
Frank Balile



No comments:
Post a Comment