nEWS: Mashirika ya kiraia yatoa tamko kwa serikali kuhusu uhakiki wa NGOs nchini...#share



WAKURUGENZI wa mashirika yasiyo ya kiserikali sambamba na Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (Nacongo) na Mtandao wa Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) wameunga mkono mchakato wa Serikali kuhakiki orodha ya mashirika hayo nchini.
 
Hivi karibuni serikali ilitangaza mchakato wa uhakiki wa mashirika yote kuanzia Agosti 21 hadi 31 mwaka huu, lengo likiwa ni kuboresha orodha ya mashirika hayo na kupima utekelezaji wa majukumu yake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, mratibu Taifa wa THRDC,  Onesmo Olengurumwa amesema wanaamini endapo zoezi hilo litafanyika vizuri litaleta manufaa kwa Taifa.

“Tunaweza kujua idadi halisi ya mashirika yanayofanya kazi na baadae kujua mchango wa mashirika hayo kwa Taifa letu kiuchumi na kijamii,” alisema Olengurumwa.

Amesema mchakato huo pia utasaidia kuondoa kwenye orodha mashirika yaliyoshindwa kuendelea kufanya kazi nchini na kubaki yale yenye tija tu.

Amebainisha kuwa kwa muda mrefu mchango wa asasi za kiraia haitambuliwi kitaifa pamoja na kwamba sekta hiyo hutoa ajira kwa watanzania wengi, kuchangia makusanyo ya kodi.

Naye katibu wa Nacongo, Ismail Suleiman amesema kutokana na mchakato huo, baraza hilo linashauri  mashirika hayo kulipa uzito suala hilo kwa kujitahidi kufika mapema katika ofisi za kanda zilizopangwa ili kufanya uhakiki katika muda uliowekwa.

Aidha ametoa rai kwa wasajili wasaidizi kote nchini kuhakikisha kuwa wanaanza kutoa barua za utambulisho kadri azaki zitakavyokuwa zikiomba kupewa barua hizo. Hiyo itayawezesha mashirika kujiandaa mapema na zoezi hilo.

Na Abraham Ntambara



About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search