Sport News: Twenzetu Gombani Leo 'kuwadeki' Yanga,.. #share (moto utawaka Leo..)

Mabingwa wa ligi kuu nchini Yanga SC walioweka kambi kisiwani Pemba kwa maandalizi ya ligi kuu na mchezo wa Ngao ya hisani, leo watatelemka dimbani kutoshana na wababe wa kisiwa hicho Jamhuri ya Pemba inayoshiriki ligi kuu visiwani Zanzibar. 



Mchezo huo utaanza majira ya saa 10 kamili jioni na kurushwa mubashara na kituo cha Azam Sports 2. 


Yanga wamekuwa katika maandalizi makali ili kujiweka sawa na msimu mpya wa ligi pia wakijidhatiti kutopoteza tena mechi ya Ngao ya hisani kama ilivyokuwa msimu uliopita mbele ya Azam FC. Sanjari na hilo ni kutopoteza mechi tatu mfululizo dhidi ya watani wao wa jadi Simba SC . Mechi ya Ngao ya hisani August 23 inawakutanisha na wapinzani wao kukiwa na utangulizi wa rekodi ya uchungu kwao kwa msimu uliokwishwa. Simba waliibamiza Yanga 3-1 kwa mikwaju ya penati katika kombe la Mapinduzi na kuendeleza tena ubabe huo katika duru la pili la ligi kuu kwa ushindi wa 2-1. 


Mechi ya leo dhidi ya Jamhuri ina mvuto wa aina yake kwa wapenzi wa timu hiyo yenye masikani yake mitaa ya Twiga Kariakoo jijini Dar es salaam wengi wakitaka kumshuhudia kiungo wao mpya toka Congo DRC Pappy Tshishimbi aliyewasili juzi kambini tayari kuitumikia klabu hiyo kwa kandarasi ya miaka miwili.


Tshishimbi ni kiungo mkabaji aliesajiliwa kutoka Mbabane Swallows ya nchini Lesotho akiaminika kuja kutibu ugonjwa kiungo cha chini ambao kwa muda mrefu umekuwa ukiisumbua klabu hiyo toka kuondoka kwa viungo bora waliowahi kuvuma na klabu hiyo; Athuman Idd ' Chuji ' na Frank Domayo .


Licha ya ukimya mkubwa wa kambi hiyo visiwani Pemba , lakini inaaminika mechi ya leo itatoa taswira ya kikosi ambacho kitashuka uwanjani jumatano ijayo kuwavaa Simba SC. Yanga inaendelea kuwakosa kikosini golikipa Beno Kakolanya, Obrey Chirwa na Geofrey Mwashiuya ambao ni majeruhi na wamebaki jijini kwa matibabu.


*Samuel Samuel*

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search