Sports News: Kuelekea 'mtanange wa Watani' wa August 23.. Tshabalala wa Simba yamkuta mazito... Azimia uwanjani kwa dakika 3... #share
KATIKA hali isiyotarajiwa, juzi usiku beki wa kushoto wa
Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, alizimia kwa zaidi ya dakika tatu baada
ya kuanguka vibaya, hali iliyolichanganya benchi la ufundi la klabu hiyo.
Hii imetokea zikiwa zimebaki siku mbili tu kabla ya timu hiyo
kukutana na mahasimu wao Yanga, katika mchezo wa Ngao ya Jamii unaotarajiwa
kuchezwa keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Ilikuwa ni katika mchezo dhidi ya Gulioni ambao Simba ilishinda
5-0, ukiwa ni ushindi wake mkubwa tangu waanze maandalizi ya msimu huu.
Beki huyo alipatwa na tatizo hilo katika dakika ya 86 baada
ya kuchezewa rafu katika eneo la 18 alipokuwa akishambulia. Alizimia na
kulazimika kufanyiwa matibabu yaliyochukua zaidi ya dakika sita palepale.
Beki huyo alianguka ghafla kisha akatulia, hatua iliyowashtua
wachezaji wenzake ambapo kiraka Erasto Nyoni, Jonas Mkude na Mwinyi Kazimoto
walimkimbilia haraka kumpa huduma kabla ya daktari wa timu hiyo, Yassin Gembe
kuingia kuokoa jahazi.
Licha ya daktari huyo kuingia kutoa msaada wa kitaalamu kwa
mchezaji huyo, mratibu wa timu hiyo, Abbas Ally na meneja Onesmo Kapinga nao
walijikuta wakiingia uwanjani bila kutarajia kwa ajili ya kuongeza msaada,
wakiwa pamoja na daktari wa Gulioni.
Hata hivyo, Tshabalala alikuwa ametulia kabisa bila ya
kutikisika huku baadhi ya wachezaji wakionekana kutaharuki, hakuweza kuitika
licha ya kuitwa zaidi ya mara tatu hadi pale fahamu zilipokuwa zimerudi na
alishindwa kumaliza mchezo huo.
Championi lilizungumza na daktari wa timu hiyo, Yassin Gembe
ambaye alisema: “Tshabalala alipatwa na mshituko kutokana na kuanguka vibaya
lakini tayari amesharejea katika hali yake ya kawaida na yupo sawa kwa kila
kitu na lile ni tukio la kawaida kwa wachezaji.”
Na Muungwana.blog




No comments:
Post a Comment