DODOMA: Bunge lapitisha Muswada wa Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2017....#share

BUNGE  leo limepitisha Muswada wa Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa mwaka 2017.

Akiwasilisha Bungeni Muswada huo leo Mjini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju amesema kuwa lengo la marekebisho yaliyopendekezwa ni kuboresha utekelezaji wa Sheria hizo kwa kuondoa upungufu uliojitokeza wakati wa kutumia sheria hizo na kuongeza masharti mengine ili kuleta uwiano kati ya Sheria zilizorekebishwa na sheria zilizopo.

"Muswada wa Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa mwaka 2017 unapendekeza kufanya marekebisho katika sheria 11 na kufuta sheria moja" amefafanua Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aidha, Masaju amesema kuwa masuala muhimu yaliyozingatiwa katika Muswada huo ni pamoja na kubadilisha vifungu vya Sheria kwa kufuta baadhi ya vifungu vya sheria hizo na kuviandika upya, kufuta baadhi ya maneno kwenye vifungu vya sheria, kuzingatia maneno mapya, kuongeza vifungu vipya na kufuta sheria moja.

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mohamed Mchengerwa amesema kuwa Kamati inashauri Serikali kuhakikisha Kamati maalumu ya kumshauri Waziri kuhusu misamaha ya kodi iundwe na wataalamu waliobobea kutoka katika fani na maeneo tofauti tofauti ili kujenga uwezo wa kamati hiyo katika kumshauri Waziri husika kuhusu misamaha hiyo ya kodi.

Kwa upande wa Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Katiba na Sheria Ally Saleh Ally amesema kuwa kambi hiyo inashauri kuwa haitoshi kuifuta RUBADA pekee bali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu malalamiko ya wananchi wanaoituhumu kupora ardhi na hatua stahiki kwa wote waliohusika zichukuliwe.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search