Hali ya Ajira Kwa Sasa Nchini Yazidi Kuwa Tete...Mgodi Huu Wapunguza Wafanyakazi...Habari Kamili Hii Hapa na Matukio360....#share

UNAWEZA ukasema sasa ajira nchini inaendelea kuwa kizungumkuti kwa vijana wengi wa kitanzania. Hii ni kutokana na Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu unaomilikiwa na Kampuni ya Acacia kupunguza wafanyakazi 2,000 kutokana na mgodi kupunguza uzalishaji.


Hatua hiyo inatokana na mgodi huo kuingia mgogoro na Serikali baada ya kuzuiwa kusafirisha makinikia kwenda nje ya nchi.

Meneja Mkuu wa Mawasiliano wa Kampuni ya Acacia, Asa Mwaipopo alisema hayo juzi wakati wa hafla ya kuwaaga wafanyakazi hao waliopunguzwa.

Mwaipopo alisema kati ya wafanyakazi 2,000 waliopunguzwa, 1,200 ni waajiriwa wa Bulyanhulu na 800 ni kutoka kwenye kampuni zenye zabuni zinazofanya kazi katika mgodi huo.

Alisema kutokana na zuio la Serikali la kusafirisha mchanga wa dhahabu (makinikia) nje ya nchi, mgodi huo umebadili mfumo wa utendaji kwa kuanzisha mtambo mpya utakaochenjua mabaki ya awali kwa kutumia kemikali ya Cyanide.

Meneja huyo alisema njia hiyo imeelezwa itatoa kiwango kidogo cha dhahabu, tofauti na uchimbaji wa awali wa mtambo mkubwa uliokuwa ukizalisha makinikia yenye dhahabu nyingi zaidi.

Hata hivyo, Acacia iliwahi kueleza kuwa kiwango cha dhahabu kinachobaki kwenye makinikia ni kidogo.

Mwaipopo alisema katika mfumo mpya wa mtambo wa uzalishaji kwa kutumia kemikali hiyo, wataajiri upya wafanyakazi 150 wa kampuni na wengine 150 kutoka kwenye kampuni zenye zabuni ambao watakuwa wakifanya usafi, ulinzi na huduma ya chakula.

Alisema mtambo mkubwa uliokuwa ukitumika kwa uzalishaji umekamilisha kazi Jumamosi, hivyo kufikia mwisho wa uzalishaji makinikia katika mgodi huo.

Mwaipopo alisema licha ya mgodi kupunguza uzalishaji na wafanyakazi, lakini ulipaji wa ushuru wa huduma kwa halmashauri na kodi za Serikali utaendelea ingawa kwa kiwango kidogo.

Kuhusu wafanyakazi waliopunguzwa, Mwaipopo alisema licha ya kuagana nao wamewapa mafunzo ya ujasiriamali na kuwaandaa kisaikolojia kwa kuwafundisha namna ya kuishi maisha mbadala tofauti na waliyokuwa nayo wakati wa ajira.

Vyama vya wafanyakazi
Mwakilishi wa vyama vya wafanyakazi katika mgodi huo, Kazimili Lubigisa alisema Jumamosi ilikuwa siku maalumu ya kumuaga Meneja Mkuu wa mgodi huo, Graham Crew lakini kwa masikitiko na hali ambayo haikutarajiwa iliwageukia wafanyakazi wote.

Lubigisa alisema kufungwa kwa mtambo huo kumesababisha madhara makubwa kwa wafanyakazi na Serikali kwa jumla, zikiwamo familia zao ambazo zimeathirika kiuchumi, elimu, afya na kisaikolojia. Pia, alisema vijiji 14 vinavyozunguka mgodi vitaathirika kiuchumi, kielimu, kiafya, miundombinu ya barabara na mapato ya Serikali.

Alisema makandarasi wanaofanya kazi katika mgodi huo nao wameathirika, hivyo ameiomba Serikali kuharakisha mazungumzo ili kuepusha madhara zaidi.
Akiwaaga wafanyakazi hao, Crew anayeondoka baada ya kufanya kazi katika mgodi huo kwa miaka miwili, alisema hakuna anayefurahia hatua iliyopo lakini akawataka kuendelea kuwa na imani kuwa mazungumzo yanayoendelea baina ya uongozi na Serikali yataleta mwafaka.

Mwananchi:


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search