Kiongozi CUF Auawa Kikatili.. Soma Habari Kamili na Matukio360..#share


Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi Chama cha Wananchi CUF Julius Mtatiro.

Ali Juma Suleiman ambaye ni Kaimu Mwenyekiti wa CUF Jimbo la Mto Pepo na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF Wilaya ya Magharibi "A" Zanzibar, ameuawa kikatili.

Kiongozi huyu wa CUF amefariki jana saa 4 usiku katika hospitali ya Mnazi Mmoja kutokana na majeraha ya kipigo cha kinyama kutoka kwa kundi maarufu sana Zanzibar linalojulikana kwa jina la "Mazombi".

Mazombi ni kikosi maalum kinachozunguka mitaani na kufanya unyama mkubwa kwa watu wasioiunga mkono CCM, hususani viongozi na wafuasi wa CUF.

Kila mara kumekuwa na matukio ya mazombi kuvamia maskani au ofisi za CUF kuwapiga na kuwaumiza vibaya viongozi, wanachama na au wafuasi wa CUF.

Kwa vyovyote vile, vyombo vya ulinzi na usalama Zanzibar vinakitambua kikosi hicho cha "Mazombi" na mikakati yake na kwa makusudi vyombo hivyo havichukui hatua yoyote.

Na zaidi ya yote vyombo vya ulinzi na usalama Zanzibar vinawafahamu viongozi wenye mamlaka wanaokitumia na kukilea kikundi hicho lakini hawawachukulii hatua zozote.

Ushenzi na unyama huu wa Mazombi hauvumiliki na natoa wito kwa wanachama na viongozi wa CUF waanze kujilinda. Haiwezekani kuendelea kuruhusu kijikundi cha wahuni kinachotumiwa na wajinga wachache kiendelee kutamba na kutoa uhai wa wananchi wasio na hatia.

Kikatiba wananchi wanalo jukumu la kujilinda hasa pale vyombo vya usalama vinapoweka vichwa mchangani na kuyaacha mazombi yatambe. Usalama wa wana CUF Zanzibar ni muhimu na njia za raia kujilinda kikatiba zinajulikana.

Naungana na watu wote waliotoa pole kwa familia ya Marehemu kulaani vikali mauaji ya kiongozi wetu. Navitaka vyombo vya ulinzi na usalama Zanzibar vitimize majukumu yake ya kulinda amani na usalama wa raia wote. Kukiacha kikundi cha wahuni kinachofahamika kiendelee kutamba mitaani na kuua watu kupigwe vita kwa nguvu zote.

Tukumbuke kuwa Zanzibar ina amani hivi sasa kwa sababu ya busara na hekima za viongozi wa CUF. Mwanya wa "uongozi bora na wa utulivu" wa CUF usitumiwe na dola kudhani kuwa wana CUF hawawezi kujilinda.

Jeshi la Polisi litoe taarifa kamili ya nani wamehusika na mauaji ya kiongozi wetu na hadi sasa wamechukuliwa hatua gani.

Mtatiro J,
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi,
28 Sept 2017.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search