Serikali Yaapa Kupigana Vita na Watu Wanaojihusisha na Mapenzi ya Jinsia Moja....#share

SERIKALI imesema inapambana kwa nguvu zote na vitendo vya mapenzi ya jinsi moja na kwamba, mwanamume atakayethibitika kufanya vitendo vya kike ataadhibiwa kisheria.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Chadema Susan Lyimo.

Mbunge huyo alisema kumekuwa na biashara kati ya wanaume na wanawake lakini pia ipo ya watu wa jinsi moja. “Nataka kufahamu hao wanachukuliwa hatua gani?” alihoji Lyimo.

Naibu waziri alisema sheria inakataza watu wa jinsi moja kufanya mapenzi  kinyume cha maumbile na pia inakataza wanaume kufanya vitendo vya jinsi ya kike.

Alisema kuna adhabu kali hutolewa na sheria hiyo kwa mtu anayebainika kufanya vitendo hivyo na kwamba, adhabu yake ni kifungo cha hadi zaidi ya miaka 30 jela.

“Tumekuwa tukipambana kwa nguvu zetu zote na makundi haya ambayo yamekuwa yakishiriki katika vitendo vya mapenzi ya jinsi moja, kuyahamasisha ama kuyahalalisha  au kuyafanya kuonekana kama ni vitu vya kawaida katika nchi yetu,” alisema.

Dk Kigwangalla alisema wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kufanya operesheni nchi nzima. Amesema taasisi mbalimbali ambazo zilikuwa na mwelekeo wa kutekeleza afua za kinga katika sekta ya afya wamezifuta na kuzibadilisha.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Costantine Kanyasu alihoji kazi ya kuwakamata wanawake wanaojiuza imefanikiwa kwa kiasi gani nchini.

Dk Kigwangalla alisema tatizo hilo ni kubwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma.

“Kitendo cha mwanamke kuishi akitegemea kipato chake au sehemu ya kipato chake kutokana na ukahaba ni kosa la kisheria,” alisema.

Naibu waziri alisema katika kutekeleza sheria ipasavyo, viongozi katika mikoa ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam wamekuwa wakikamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ya wanawake wanaojiuza.

Alisema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wataendelea kuhakikisha wanawake wanaojihusisha na biashara hiyo wanaendelea kukamatwa ili kulinda heshima, utu na hadhi ya wanawake wa Tanzania.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search