Serikali Yawakaribisha Wawekezaji wa Anga Nchini...Habari Kamili Hii Hapa na Matukio360....#share
SERIKALI imesema inawakaribisha wawekezaji wa sekta ya anga kuja kuwekeza nchini ili kukuza utalii na kuitoa nchi kutoka uchumi wa kati kwenda uchumi wa viwanda.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Anga lililokutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo.
Amesema sekta ya anga ni muhimu katika maendeleo ya uchumi wa nchi na kwamba usafiri wa anga ukiboreshwa utasaidia watalii wengi kuja nchini na kuchangia pia katika maendeleo ya viwanda huku akisisitiza Serikali haitakuwa tayari kupokea wawekezaji wababaishaji.
"Milango iko wazi kwa wawekezaji tunawahitaji kwa maendeleo ya nchi ila hatutakubali kuwapa wawekezaji wababaishaji tunataka wanaoeleweka na wenye nia ya kweli ya kuwekeza," amesema Profesa Mbarawa.
Amebainisha kuwa sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za ukosefu wa marubani,mafundi na wahandisi wa ndege na kwamba Serikali inajipanga kuondoa tatizo hilo kwa kuimarisha ujenzi wa viwanja vya ndege na utoaji wa taaluma ya urubani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL),Ladislaus Matindi amesema hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Septemba kutakuwa na marubani 20, mafundi 36 na wahandisi 27 huku akiongeza kufikia mwakani matarajio marubani watafika 50, wahandisi 50 na mafundi 126.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Aviation University College, Chalanga Kejeli ameitaka jamii kuondokana na dhana kuwa masomo ya anga yanasomwa na watu wenye uwezo mkubwa badala ni masomo yanayoweza kumudiwa yakiwekewa nia madhubuti.
Ameiomba Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini(Heslb) kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaopenda kusoma masomo ya anga ili wanataaluma hiyo waongezeke na kuchangia ajira.
Na Husssein Ndubikile
No comments:
Post a Comment