THTU yaendelea kuelimisha jamii kushiriki kwenye mchakato wa bajeti na mipango..
JAMII imeshauriwa kujenga utamaduni wa kuhudhuria mikutano inayohitishwa na Viongozi wa Serikali za Mitaa ili iweze kupata taarifa mbalimbali za mapato na matumizi, kuibua changamoto zinazowakabili na vipaumbele.
Ushauri huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mchumi kutoka Manispaa ya Ilala, Lucy Kayombo wakati wa Semina ya Mafunzo inayotolewa na Taaasisi ya Tanzania Higher Learning Institution Trade(THTU) yenye lengo la kuielimisha jamii kushiriki kwenye mchakato wa bajeti na mipango
Amebainisha kuwa viongozi wamekuwa wakitelekeleza jukumu lao kuwajulisha wananchi masuala ya msingi ikiwemo utangazaji wa mikutano ya kujadili miradi ya maendeleo ila cha kushangaza hawashiriki vikao na mikutano huku akisisitiza hulalamikia mambo yaliyopitishwa kwenye mikutano hiyo.
'' Ni muhimu wananchi kuhudhuria mikutano ya mitaa wengi wao hawashiriki hata masuala yanajadiliwa huko hawayajui linapokuja suala la utekelezaji wanalalamika,'' alisema Lucy.
Kayombo amesema kupitia mikutano hiyo wananchi watapata fursa za kuhoji usomaji wa taarifa ya mapato na matumizi yanayotakiwa kusomwa na viongozi pamoja na kujadili ujenzi wa miradi yenye tija kwenye maeneo yao ikiwemo ujenzi wa shule, masoko na hospitali.
Ameongeza kuwa endapo watashiriki kikamilifu watapata fursa za kuainisha na kukataa mambo yasiyo ya msingi yanayotaka kupitishwa bila ridhaa yao.
Pia amesema changamoto kubwa inayochangia tatizo hilo inatokana na wananchi hawajajengewa uwezo wa kushiriki masuala ya msingi yanayowahusu.
Kwa upande wake Mratibu Mkuu wa mradi na mafunzo hayo, Emiliana Mbwiga amesema mafunzo hayo yalianza kutolewa kwa viongozi kuanzia ngazi halmashauri,wilaya na kata huku akibainisha mwishoni watakutana tena na viongozi kuwajulisha wawakilishi wao walichokijadili.
Amesema mradi huo unafadhiliwa na Taasisi ya The Foundation for Civil Society na kwamba mafunzo hayo kwa asuilimia kubwa yatawasaidia kujua haki zao za kuhoji na kushiriki mambo yanayofanyika katika mitaa na kata zao.
Naye Mratibu Msaidizi wa mradi ambaye pia ni mwezeshaji, Memory Njakile amesema ushiriki mdogo wa wananchi katika mikutano hiyo husababisha utekelezaji wa ukusanyaji wa fedha za kuzolea taka na za ulinzi shirikishi kuwa mgumu.
No comments:
Post a Comment