Waziri Mwijage Mgeni Rasmi Maadhimisho Tamasha la Wanawake Wajasiriamali..Habari Kamili na Matukio360..#share

Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage  anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Tamasha la Wanawake Wajasiriamali(Mowe) litakalofanyika kuanzia Oktoba 24 hadi 30 mwaka huu katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo jijini humo na Mwenyekiti wa Mowe, Zubeda Kiluwa wakati akitoa ufafanuzi kwa wanahabari juu ya taratibu na mpangilio mzima wa tamasha utakavyokuwa.

Amesema  Waziri Mwijage ndiye atakayefungua maadhimisho hayo huku akisisitiza lengo kuu  la tamasha hilo ni kuwahamasisha wanawake kujishughulisha na shughuli za kiuchumi za kuwaingizia kipato kwa kutumia fursa za kibiashara na rasilimali zilizopo.

“Wanawake wote popote walipo waje washiriki siku hiyo  wataonyesha na kutangaza bidhaa na huduma mbalimbali wanazozifanya kwa lengo la kupanua wigo wa masoko,” amesema Kiluwa.

Amesisitiza kuwa wanawake wajasiriamali watapata fursa ya kujifunza na kukabiliana na ujuzi na uzoefu wa stadi mbalimbali na kwamba tamasha hilo limebeba kauli mbiu inayosema  ‘Mwanamke Mjasiriamali funguka shiriki kujenga Tanzania ya Viwanda’.

Aidha, amesema washiriki wa tamasha hilo watatakiwa kulipa gharama ya ushiriki sh 50,000 na kuwataka wananchi wajitokeze kwa wingi katika viwanja hivyo ili waweze kujionea bidhaa zinazozalishwa na wanawake hao.

Amebainisha kuwa tamasha hilo halitahusisha wanawake wajasiriamali kutoka nchini pekee bali wengine watatoka nchi jirani za Kenya, Uganda, Burundi, na Rwanda pamoja na mataifa mengine ya Afrika.

Na Hussein Ndubikile


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search