Afya ya Harbinder Sethi bado 'tete'...soma habari kamili na Matukio360...#share

Na mwandishi wetu
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa mshtakiwa Harbinder Sethi pamoja na  kupelekwa  Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH) na kuchukuliwa vipimo bado hajapata majibu wala matibabu yoyote na afya yake inazidi kuzoofika.


Harbinder Sethi wa pili kutoka kushoto
Wakili wake, Alex Balomi leo ameeleza  hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,  Huruma Shaidi Mara baada ya Wakili wa Serikali  Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine.

Kishenyi baada ya kueleza hayo, Wakili Balomi  alieleza kuwa kwa kiasi fulani upande wa Mashtaka umetekeleza amri ya mahakama kwa kumpeleka Muhimbili na kuchukuliwa vipimo lakini hajapewa majibu na wala hajatibiwa hadi sasa.

Amedai kuwa lile puto alilowekewa tumboni Sethi linatakiwa kubadilishwa mwishoni kwa mwezi huu, lisipobadilishwa litageuka kuwa sumu na kuhatarisha uhai wake.
Aliendelea kudai kuwa daktari aliyechukua vipimo ampatie majibu ili aweze kujua hali ya afya yake ikoje.

Wakili Kishenyi baada ya kutolewa kwa maelezo hayo alidai kuwa wao wamekwisha tekeleza  amri ya mahakama, hawana cha kufanya zaidi kwa sababu majibu ni siri ya magonjwa na Daktari.

Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Takukuru, Leonard Swai yeye naye alidai kuwa suala la majibu ni suala la magonjwa na Daktari.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Shaidi Alisema amri ya mahakama imetekelezwa ambapo mshtakiwa alipelekwa Muhimbili, na siyo jukumu la mahakama kuingilia kazi ya Daktari hivyo alishauri mawakili wa upande wa utetezi wafuate utaratibu.

Kesi imeahirishwa hadi Novemba 10,2017 kwa ajili ya kutajwa na kuusisitiza upelelezi ukamilishwe.
Wakili wa  mshtakiwa James Rugemalira, Respicius Didas aliunga mkono hoja za wakili Balomi na kuongeza  kuwa kuna suala la ucheleweshwaji wa upelelezi  katika kesi hiyo.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa Mara ya kwanza  Juni 19,mwaka 2017 na wapo ndani hadi sasa.
Katika kesi hiyo, washtakiwa Harbinder  Singh Sethi na James Burchard  Rugemarila wanakabiliwa na  mashtaka 12 ya  uhujumu uchumi kwa  Kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kighushi, kutoa nyaraka za kughushi na  kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.

Pia wanakabiliwa na mashtaka matano ya  kutakatisha fedha pamoja na  kusababisha hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.


Rugemarila ni  Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL na Sethi ni Mwenyekiti Mtendaji wa PAP ambapo  wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya oktoba 18 ,2011 na Machi 19 , 2014.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search