Sheikh Ponda awatoroka Polisi kikomando...Waandishi watatu wakamatwa ..#share


NI kama Filamu, Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia Sheikh Issa Ponda kuwatoroka askari polisi  zaidi ya kumi waliotaka kumkamata.

Sheikh Issa Ponda akizungumza na waandishi wa habari 

Tukio hilo limetokea leo majira ya saa tano asubuhi jijini Dar es Salaam katika hoteli ya Iris baada ya  askari polisi kuvamia katika mkutano wa waandishi ambapo Sheikh Ponda alikuwa akitoa taarifa mbalimbali kutokana na matukio yanayoendelea ikiwamo mwenendo mzima wa mauaji, maiti kuokotwa, raia na viongozi kadhaa kutekwa na kupotea.

‘’Inaonekana baadhi ya askari polisi  hawamfahamu sheikh Ponda kwani amewapita hapa wakiwa wanarandaranda na kutoka nje na kutokemea upande wa kulia wa hotel ya Iris.’’
Shuhuda amesema Sheikh Ponda alipishana na baadhi ya askari wanne ambao ndio wanaomjua vizuri kwa yeye kutumia  njia ya miguu (ngazi) huku askari kanzu  wakitumia               lifti hotelini hapo.

Awali katika mkutano huo, Sheik Ponda alisema Watanzania wamekata tamaa na usalama wao  na wanaishi kwa hofu na kwamba kama Serikali inawajibika ipasavyo matukio hayo yasingekuwepo.

‘’Serikali imekuwa ikiwaandama baadhi ya viongozi wa dini na wa vyama vya siasa hasa vya upinzani, wakati  viongozi hao ndiyo wanaoikumbusha serikali wajibu wake na sasa  wamekuwa wakifikwa na hatari ikiwamo kupata vilema vya kudumu.’’ Na kuongeza ‘’Mimi binafsi nilipigwa risasi hadharani mwaka 2013  na hivi sasa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Tundu Lissu .’’

Pia Sheikh Ponda ameiomba Serikali kuacha kuwazuia viongozi wa upinzani kuzungumza mambo mbalimbali yahusuyo nchi.

‘’Serikali imezuia haki za kidemokrasia kwa viongozi wa upinzani. Imezuia kufanya mikutano ya hadhara na maandamano ya amani.’’

 Awali Polisi walifika hotelini hapo wakiwa na gari mbili aina ya Defender wakiwa na silaha za moto kwa lengo la kumkamata Sheikh Ponda na kumzuia asizungumze na waandishi wa habari.

Wakati huo huo,  waandishi watatu kutoka vyombo mbalimbali vya habari   walikamatwa na polisi hao  na kupakiwa garini na kupelekwa mahala kusikojulikana.
Kukamatwa kwao kulitokana na hatua yao ya kuwapiga picha polisi na gari zao na pia   kuangali kilichozungumzwa na Sheikh Ponda.

Hata hivyo wakati tunarusha habari hii, waandishi hao waliachiwa huru baada ya kushikiriwa kwa  saa tatu

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search