Tanesco Walia na Vishoka, 116 Wadakwa Wakitumia Umeme Bure..Soma Habari Kamili na Matukio360..#share
Na Salha
Mohamed
SHIRIKA la Umeme nchini (Tanesco), limepata
hasara zaidi ya Sh. Mil 116 kwenye operesheni ya kukagua mita za umeme kwa
wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam huku wateja 116 wakikamatwa kwa kutumia umeme bure.
Fundi Umeme wa shirika la Tanesco, Zuberi Kediga, akiwa juu ya moja ya nyumba ya Mteja maeneo ya Tegeta akikata waya wa umeme baada ya kubaini kuiba umeme kinyume na sheria wakati wa Oparesheni inayoendelea jijini Dar es Salaam. Mteja huyo aliyekuwa akiiba umeme. Picha na Prona Mumwi
Operesheni hiyo endelevu imeanza Septemba 26
mwaka huu, imewafikia wananchi 5,444 ikiwa na lengo la kuangalia miundombinu ya
Shirika hilo kwa Kanda ya Mkoa huo kwa kila mtumiaji wa umeme.
Akizungumza jana wakati wa Operesheni hiyo,
Mhandisi Mkuu Mkaguzi na Udhibiti wa Mapato Kanda ya Dar es Salaam na Pwani,
Mrisho Sangiwa amesema kati ya watumiaji 5,444 wa umeme, mita 49 zimekutwa hazitumii
umeme vizuri.
“Tumebadilisha mita zaidi ya 100. Tukiangalia
mahesabu yaliyopatikana kwa wateja waliokuwa wanamatatizo ni zaidi ya sh. Mil
166 hadi leo(jana) na robo ya pesa hizo zimeshalipwa,”amesema.
Amesema Operesheni hiyo itafika kwa kila
mtumiaji wa umeme mkoani humo na Pwani, ambapo mteja atakayekutwa akiiba umeme
atachukuliwa hatua za kisheria kwani wizi wa umeme ni kosa kwa kuingilia
miundombinu ya Shirika kwani sheria ya umeme ya 2008 imebainisha.
Mhandisi Sangiwa amesema wananchi wanapaswa kuepuka
vishawishi vya vishoka kwa kuwaunganishia umeme bure kwani kunaweza kusababisha
mlipuko na kuuunguza nyumba na kubainisha kuwa wakikamatwa gharama zake ni
kubwa hivyo watumie umeme kulingana na matumizi yao.
Amesema
miundombinu ya umeme ni gharama wananchi wanapaswa kuipenda ili kulipa kodi
serikalini kwa kulipa bili na hata kusaidia wananchi wasiokuwa na umeme
kuunganishiwa nishati hiyo hadi vijijini.
Ameongeza kuwa kwa sasa wanaendelea kutoa elimu
kwa wananchi kwani wengi hawana elimu ya matumizi sahihi ya vifaa
vya umeme na matumizi yake, muda wa kifaa hicho(uchakavu)
na si kuvilalamikia ubora wake.
“Wananchi tuungane kupiga vita wizi wa umeme, na
huu mchakato ni endelevu,msishawishiwe na vishoka kwa kuwawekea umeme bure,
vishoka ni mafundi umeme wengi hawajasajiliwa, wananchi wawe makini,”amesesma.
Ameongeza kuwa wapo vishoka wanaojifanya kukagua
miundombinu ya umeme majumbani kwa
kuwatengenezea lakini bnaadae humwambia kishoka mwenzie na kujitambulisha kama
ni ofisa kutoka Tanesco na kukagua ili kujipatia fedha.
Mhandisi Sangiwa amewataka wananchi kudai
vitambulisho endapo atakuja mkaguzi wa kukagua miundombinu ya umeme ambapo kama
mteja atakuwa na wasiwasi asisite kupiga simu Tanesco ili kuchukuliwa hatua.
Ametoa wito kwa wananchi kuwa wazalendo kwa
kulinda miundombinu ya umeme ili kutekeleza
sera ya uchumi wa viwanda na kulijenga taifa na kutoa taarifa kwa wanaokiuka taratibu
na sheria za shirika hilo kwa kupewa zawadi.
Fundi Umeme wa Shirika la Tanesco, Issaya Haule, akionesha waandishi wa habari mita iliyochezewa na vishoka katika moja ya nyumba iliopo eneo la Tegeta mtaa wa Panga Dar es Salaam.
Mhandisi Mkuu Mkaguzi Udhibiti wa Mapato Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Mrisho sangiwa, (kushoto) akitoa maelezo kwa mafundi na maofisa wa Shirika la Tanesco kuhusu oparesheni ya ukaguzi wa mita.
Moja ya nyaya zilizounganishwa kwa wizi wa umeme
No comments:
Post a Comment